Jun 22, 2016 17:16 UTC

Baada ya kusambaratisha njama za magaidi wa kitakfiri waliotaka kufanya mashambulio mjini Tehran, Wizara ya Usalama wa Ndani ya Iran imesambaza mkanda wa video unaoonesha sehemu moja ya operesheni ya kutiwa mbaroni magaidi hao wakiwa katika maficho yao mjini Tehran.

Mkanda huo umesambazwa leo Jumatano na unaonesha askari wa Iran wakiingia katika jengo moja kwa kuchupa ukuta na kuwatia mbaroni baadhi ya magaidi hao ambapo mmoja alikamatwa akiwa usingizi.

Vile vile inaonesha gari aina ya Peugeot 405 ikiwa imeshategwa mabomu kwa ajili ya kuripuliwa.

Jana Jumanne, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran Mahmoud Alavi aliwaambia waandishi wa habari kuwa kundi hilo la magaidi zaidi ya 10 walitiwa mbaroni katika kipindi cha baina ya Juni 14 hadi 20 mjini Tehran, katika maeneo matatu ya mpakani na kwenye mikoa ya katikati mwa Iran.

Alavi ameongeza kuwa, magaidi hao walikuwa wamepanga kuripua mabomu ya kuongozwa kwa mbali, mabomu ya kujiripua na magari yaliyotegwa mabomu katika maeneo yenye mjumuiko wa watu wengi, katika sehemu 50 tofauti nchini Iran.

Tags