Manowari za IRGC zasimikwa makombora yanayopiga kilomita 2,000
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) amesema jeshi hilo la SEPAH kwa mara ya kwanza limeanza kuzisheheneza manowari za Iran kwa makombora yaliyoundwa na wataalamu wa hapa nchini, yenye uwezo wa kupiga shabaha umbali wa kilomita 2,000.
Meja Jenerali Alireza Tangsiri alisema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, makombora hayo yamesimikwa kwenye meli ya kijeshi iliyoundiwa hapa nchini na kupewa jina la Shahid Soleimani. Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, alikuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC aliyeuawa kigaidi na Marekani Januari 3, 2020.
Kamanda huyo wa IRGC amesema, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyopata ushindi mwaka 1979, Iran ilikuwa ikimiliki makombora yasiyopiga shabaha zaidi ya kilomita 40, lakini hii leo inaona fahari kubwa kumiliki makombora yanayopiga hadi kilomita 2,000, pasi na kutegemea msaada wa maajinabi.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kupata mafanikio haya yote ya kujizalishia manowari za kijeshi na makombora ya kisasa yenye uwezo mkubwa, licha ya vikwazo na mashinikizo ya kiuchum ya maadui wa taifa hili.
Meja Jenerali Alireza Tangsiri hivi karibuni alionya vikali kuwepo kwa jeshi la Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa kisingizio cha kulilinda eneo hilo la kistratijia la baharini. Alisema Iran inaziona meli za kijeshi za Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa lake na chanzo cha mivutano na ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.
Akthari ya meli za kijeshi za Iran zilizoundwa kwa teknolojia na wataalamu wa hapa nchini, zimesheheni mifumo ya kisasa yenye uwezo wa kuvurumisha makombora ya chini ya maji (torpedo).
Jeshi la Majini la Iran mbali na kulinda maji ya taifa hili, lakini pia limezima mara kadhaa mashambulizi ya maharamia dhidi ya meli za mizigo na mafuta za nchi hii na nchi nyingine katika maji ya kimataifa.