Aug 23, 2023 02:36 UTC
  • OIC yatoa wito wa kulindwa Msikiti wa Al-Aqsa

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeisitiza umuhimu wa kulindwa hadhi ya kihistoria na kisheria ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo huko al-Quds (Jerusalem).

Katika taarifa, OIC imelaani ukiukaji unaoendelea kufanywa dhidi ya Msikiti unaoheshimika wa Al-Aqsa mjini al Quds na kusisitiza udharura wa jamii kimataifa kuingilia na kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unavamia mara kwa mara eneo hilo takatifu.

Taarifa ya OIC imesisitiza kwamba Msikiti wa Al-Aqsa na jengo lake kubwa ni mahali pa ibada kwa ajili ya Waislamu pekee.

Taarifa hiyo pia imeadhimisha kumbukumbu ya miaka hamsini na nne ya kuchomwa moto Msikiti wa Al-Aqsa, ikiwa ni Kibla cha kwanza cha Waislamu na eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu baada ya Makka na Madina.

Huku kukiwa na hali ya kuongezeka ukiukwaji wa sheria unaofanywa na Israel na juhudi zake za mara kwa mara za kudhoofisha hadhi ya msikiti huo, OIC imeashiria uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali, mara nyingi wakilindwa na askari vamizi wa Israel.

Askari wa utawala haramu wa Israel wakiwa wanatekeleza uvamizi dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa

Vitendo hivi vimesababisha kuvunjiwa heshima  eneo hilo takatifu, kufungwa kwa malango yake, na mashambulizi ya kinyama dhidi ya waumini Waislamu.

Shirika hilo limesisitiza kuwa Al-Quds Al-Sharif yaani Jerusalem, ni sehemu muhimu ya ardhi ya Palestina iliyotekwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka wa 1967. OIC imepinga kikamilifu majaribio au maamuzi yoyote yaliyolenga kubadilisha idadi ya watu au sifa za kijiografia za eneo hilo.

Taarifa hii imetolewa kwa mnasaba wa siku ya Agosti 21, ambayo ni Siku ya Msikiti Duniani. Sababu iliyopelekea siku hii kutengwa kama Siku ya Kimataifa ya Misikiti inahusiana na tukio lililotokea miaka 56 iliyopita katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Katika tukio hilo la kusikitisha, Mzayuni mwenye itikadi kali kwa jina Dennis Michael William Rohan aliuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa katika hatua iliyopangwa vyema na kuungwa mkono na serikali ya wakati huo ya utawala haramu wa Israel.

Tags