Dec 23, 2023 08:18 UTC
  • Azimio la Baraza la Usalama kuhusu Gaza: Ni hatua ya lazima lakini haitoshi

Ijumaa ya jana, Desemba 22, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuongeza misaada ya kibinadamu kwa watu wa Ukanda wa Gaza bila kutoa wito wa kusitishwa mapigano. Marekani na Russia, wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama, hazikulipigia kura azimio hilo. Wajumbe wengine 13 wamelipigia kura ya ndiyo.

Akizungumzia azimio hilo, mwakilishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika Umoja wa Mataifa amesema: "Azimio lililowasilishwa na UAE linataka kuongezwa misaada ya kibinadamu huko Gaza na kuteuliwa mratibu wa masuala ya kibinadamu ili kurahisisha operesheni za kuingizwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza."

Marekani ilipiga veto ombi la Russia la kujumuisha kifungu cha "kukomesha uhasama mara moja na daima" katika maandishi ya azimio hilo. Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya, amesema: "Washington inacheza mchezo mbaya wa kutoa leseni inayoiruhusu Israel kuwaua raia wa Palestina."

Vasily Nebenzya

Gilad Erdan, mwakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa amepinga azimio hilo na kudai kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kujikita kwenye mfumo wa kutuma misaada huko Gaza si jambo la dharura na inakwenda kinyume na ukweli wa mambo.

Katika upande mwingine, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelitaja azimio hilo la Baraza la Usalama la UN kuhusu Gaza kuwa ni "hatua ambayo haitoshi" kwa ajili ya kukomesha mapigano na kushughulikia mgogoro wa binadamu huko Gaza. Taarifa ya Hamas imesema kwamba, Baraza la Usalama lina wajibu wa "kuhakikisha kiasi cha kutosha cha misaada ya kibinadamu kinawasili katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, hasa katika maeneo ya kaskazini." Hamas pia imesema kuwa azimio la Baraza la Usalama lilipaswa kutoa wito wa kusitishwa mara moja operesheni za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Gaza.

Azimio hilo limeidhinishwa baada ya upigaji kura juu yake kiahirishwa mara nne katika siku kadhaa zilizopita. Hatimaye, jana Ijumaa mwakilishi wa Marekani alitangaza kwamba yuko tayari kuupigia kura muswada mpya na uliorekebishwa wa azimio hilo. Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba, Washington imekuwa ikiunga mkono kikamilifu operesheni za kijeshi na mashambulizi yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Watoto na wanawake wa Gaza wanaendelea kuuawa na Israel kwa msada wa Marekani.

Katika upande wa kisiasa na kidiplomasia pia, Marekani imepinga maazimio kadhaa yaliyotaka kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza na imebariki mashambulizi hayo kwa kisingizio cha eti haki ya kujilinda ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wakati huo huo, wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi za serikali ya Washington kama Wizara ya Mambo ya Nje, Idara ya Usalama wa Taifa na hata wafanyakazi wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, wamekuwa wakimtaka Joe Biden aishinikize Tel Aviv ili isitishe mashambulizi ya kikatili yanayoua shahidi na kujeruhi maelfu ya watu wa Gaza, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Ijapokuwa mkwamo wa kupitishwa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Gaza hatimaye umevunjwa, lakini suala la msingi, yaani kuulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel kusitishwa vita vya Gaza, bado linaendelea kupuuzwa. Suala hili limezingatia sharti lisiyo halali na la kidhalimu la Marekani, yaani kutojumuisha takwa lolote la kusitisha mapigano katika rasimu ya azimio la UN ili liweze kuidhinishwa.

Suala hili limekosolewa na kupingwa na wajumbe wa Baraza la Usalama na mashirika ya kutetea haki za binadamu. Vasily Nebenzya, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, ametangaza kwamba Moscow haikupiga kura ya veto dhidi ya azimio jipya la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukanda wa Gaza kwa sababu tu ya kuonyesha mshikamano na nchi za Kiarabu. Hasa ikizingatiwa kwamba, Moscow ilipendekeza kujumuisha kifungu cha "kukomesha mapigano mara moja na daima" katika muswada wa azimio hilo, ambacho kilipingwa kwa kura ya veto ya serikali ya Washington.

Kaburi la umati la raia wa Gaza waliouawa na Israel

Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yamekosoa azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo halitoi wito wa kusitishwa mapigano Ukanda wa Gaza. Jason Lee, Mkurugenzi Mtendaji wa Save the Children, amesema kuwa hatua yoyote isiyokuwa ya kutoa wito wa kusitishwa mapigano inazidisha mateso ya mauaji, magonjwa, na njaa kwa watoto wa Gaza. Shirika la Oxfam pia limetangaza kwamba kutowekwa kifungu cha ulazima wa kusitishwa vita katika azimio hilo baada ya kuahirishwa upigaji kura kwa siku tano katika Baraza la Usalama "ni jambo lisiloeleweka na la kikatili kabisa."

Tags