Jan 30, 2024 02:44 UTC
  • Sababu za Israel kupenda vita vienee eneo zima la Asia Magharibi

Duru mbalimbali za habari zimeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya njama za kila namna za kutaka vita vienee kwenye eneo zima la Asia Magharibi.

Jumamosi usiku, televisheni ya LBC ya Lebanon ilinukuu duru za kuaminika zikisema kuwa, maafisa usalama wa baadhi ya nchi za Kiarabu wameyaonya makundi ya muqawama ya Lebanon kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel unajiandaa kuivamia na kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni navyo vimeripoti kuwa, maelfu ya wanajeshi wa kikosi cha Golan cha Israel ambao wameondoka Ukanda wa Ghaza wamepelekwa kwenye mpaka wa kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazopakana na Lebanon wakiwa pamoja na mamia ya vifaru. Amma swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kitu gani kinaufanya utawala wa Kizayuni upende kuona eneo zima la Asia Magharibi linanea vita?

Sababu ya kwanza inatokana na serikali yenyewe iliyoko madarakani huko Israel. Serikali hiyo inayoongozwa na Benjamin Netanyahu imejaa Wazayuni wenye misimamo mikali ambao wanapenda mno vita. Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa Israel ni miongoni mwa Wazayuni wenye misimamo mikali mno ambaye hivi karibuni aliiambia kanali ya 14 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni kuwa, anatamani kuona jeshi la utawala wa Kizayuni linaingia vitani na Hizbullah ya Lebanon na vita vya Ghaza navyo vinaendelea bila ya kusita.

Tukija kwa Netanyahu mwenyewe uhakika wake ni kuwa anaamini kwamba uwepo wake wa kisiasa unategemea kikamilifu kuendelea vita na kutokomeshwa mapigano huko Ghaza kwani anaamini kwamba kumalizika vita vya Ghaza maana yake ni kumalizika maisha yake ya kisiasa. 

Sababu nyingine inahusiana na hatua zinazochukuliwa na Hizbullah ya Lebanon katika kuwaunga mkono ndugu zao wa Palestina hasa wa Ukanda wa Ghaza. Siku chache baada ya Israel kuanzisha vita vikubwa na vya pande zote dhidi ya Ghaza hapo tarehe 7 Oktoba, Hizbullah ya Lebanon ilianza kuushambulia utawala wa Kizayuni katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel. 

Sababu nyingine ni kwamba utawala wa Kizayuni unaamini kuwa Hizbullah ya Lebanon inaogopa kuingia kwenye vita vikubwa kwani inahofia mazingira yanayotawala hivi sasa nchini Lebanon. Sasa hivi nchi hiyo ya Kiarabu imo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi na katika upande wa kisiasa pia hadi hivi sasa hitilafu za ndani zimezuia kuchaguliwa rais na waziri mkuu mwingine wa nchi hiyo.

Wazayuni wanaamini kuwa, ni kwa sababu hiyo ndio maana Hizbullah ya Lebanon inaogopa kuingia kwenye vita vya pande zote na utawala wa Kizayuni katika miezi ya hivi karibuni. Kwa mtazamo wa viongozi wa Israel, msimamo wa Hizbullah ya Lebanon unadhoofishwa na masuala ya ndani ya Lebanon, hivyo Israel ina nia ya kuanzisha vita vipya dhidi ya Lebanon na halafu lawama zote iisukumie harakati ya Hizbullah. 

Ben Gvir, Mzayuni mwenye chuki na uadui mkubwa na Waislamu na binadamu

 

Mtazamo huo wa viongozi wa utawala wa Kizayuni umejitokeza katika hali ambayo hata ndani ya utawala wa Kizayuni kwenyewe, watu wengi wanamuonya Netanyahu na genge lake la wapenda vita linalounda serikali ya Israel, kwamba, wasithubutu kabisa kuingia vitani na Hizbullah ya Lebanon.

Sababu nyingine inayowafanya viongozi wa Israel wapende vita vienee kwenye eneo zima la Asia Magharibi ni kwamba, tangu ilipoanza opereshenei ya Kimbunga cha al Aqsa, muda wote utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya njama za kuitumbukiza moja kwa moja Marekani kwenye vita. Inavyoonekana ni kuwa viongozi wa utawala wa Kizayuni wanataka vita vienee kwenye eneo hili zima ili kuilazimisha Washington iingie moja kwa moja vitani. 

Jengine ni kwamba utawala wa Kizayuni unataka kuitumbukiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye vita vya moja kwa moja. Lakini uhakika wa mambo ni kuwa, iwapo Wazayuni watachochea kuenea vita kwenye eneo hili zima, wa kwanza kabisa atakayeangamia na kupata madhara makubwa zaidi ni utawala wa Kizayuni wenyewe kabla ya upande mwingine wowote. 

Tags