Feb 26, 2024 11:47 UTC
  • Mkuu wa UNRWA: Janga la njaa la 'kutengezwa na watu' Ghazza linaepukika kwa kuruhusu kuingizwa misaada

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema baa la njaa kali lililozagaa katika Ukanda wa Gaza linaweza kuepukwa ikiwa misaada itaruhusiwa kuingizwa katika eneo hilo.

Philippe Lazzarini ameeleza katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X kwamba, mara ya mwisho UNRWA ilipoweza kupeleka msaada wa chakula kaskazini mwa Ghazza ni tarehe 23 Januari.
 
Lazzarini ameongezea kwa kusema: "tangu wakati huo, sisi pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, tumetoa indhari kuhusu njaa inayozidi kuongezeka, tukaomba misaada ya kibinadamu ifikishwe kila wakati, na tukasema kwamba njaa inaweza kuepukwa ikiwa misafara zaidi ya chakula itaruhusiwa kwenda kaskazini mwa Ghazza".
Philippe Lazzarini 

Kamishna wa UNRWA ameeleza kuwa miito yao ya kupelekwa msaada wa chakula huko Ghazza imekataliwa na kuangukia kwenye masikio ya viziwi.

 
Lazzarini ameeleza bayana kuwa janga hilo ni la kutengenezwa na watu akikumbusha kuwa ulimwengu uliahidi kutoruhusu baa la njaa litokee tena na akaongezea kwa kusema, janga la njaa huko Ghazza lingali linaweza kuepukwa kupitia utashi wa kweli wa kisiasa utakaowezesha kufunguliwa njia na kutoa ulinzi ili kufikisha misaada athirifu.
 
Kamishna Mkuu wa UNRWA amesema: "siku zijazo zitautahini tena ubinadamu wetu na thamani zetu za kiutu."
 
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshtakiwa kufanya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ). Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama hiyo mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inatolewa na kufikishwa kwa raia huko Ghazza.../

 

Tags