Mar 07, 2024 02:30 UTC
  • Muqawama wa Iraq waendeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya Wazayuni + VIDEO

Makundi ya muqawama wa Kiislamu ya Iraq yametangaza kuwa yameendelea kuyashambulia maeneo mbalimbali ya utawala wa Kizayuni kwa kutumia droni (ndege zisizo na rubani) na kwamba mashambulizi hayo yataendelea hadi Israel itakapokomesha mashambulio yake dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Shirika la habari la IRIB lilitangaza habari hiyo jana Jumatano na kuongeza kuwa, mashambulizi hayo ya Waislamu wa Iraq dhidi ya Israel yamefanyika kuwaunga mkono ndugu zao wa Palestina hasa wa Ukanda wa Ghaza ambapo wapiganaji jihadi wa Iraq wameshambulia kinu cha umeme na uwanja wa ndege wa Haifa ndani ya ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Siku mbili zilizopita pia, makundi ya muqawama ya Iraq yalitumia droni kukipiga kwa makombora kituo cha kemikali cha bandari ya Haifa ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

 

Kwa muda wa miezi mitano sasa utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na mbele ya macho ya walimwengu. Hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 30,000 wameshauawa shahidi na zaidi ya 70,000 wengine wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kijinai ya Israel dhidi ya raia hao wasio na ulinzi.

Amma katika upande wa kutimuliwa wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq, Bw. Ibrahim al Sikini, mjumbe wa Mrengo wa Serikali ya Kisheria ya Iraq amesema baada ya kutozaa matunda mazungumzo ya kisiasa baina ya Iraq na Marekani kuhusu kutimuliwa nchini humo wanajeshi vamizi wa kigeni kwamba, Washington inaendelea kupoteza muda kupitia mbinu mbalimbali kama ya kuundwa kamati ya pamoja ya kufuatilia suala la kufurushwa wanajeshi wake nchini Iraq.

Tags