Mar 17, 2024 08:17 UTC
  • Makundi ya mapambano ya Palestina yakosoa hatua ya Mahmoud Abbas ya kumteua waziri mkuu mpya

Mahmoud Abbas, Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, amemteua Mohammad Mustafa kwa ajili ya kuunda baraza jipya la mawaziri, hatua ambayo imekosolewa na makundi ya muqawama ya Palestina.

Awali, Waziri mkuu wa zamani wa Palestina, Mohammad Ashtiyeh, alikuwa amejiuzulu ambapo Mahmoud Abbas akakubali kujiuzulu kwake lakini akamuomba aendelee kubakia kwenye nafasi hiyo hadi wakati wa kuundwa baraza jipya la mawaziri. Waziri mkuu mpya wa Palestina ameteuliwa katika hali ambayo vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza vinavyoendeshwa na utawala ghasibu wa Israel vimeingia katika mwezi wa sita, vita ambavyo kufikia sasa vimepelekea Wapalestina wapatao 32,000 kuuawa shahidi na wengine zaidi ya 73,000 kujeruhiwa. Hata hivyo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina bado haijachukua hatua yoyote ya kuwatetea watu wa Gaza.

Licha ya kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekuwa ikizitaja jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Gaza kuwa ni mauaji ya halaiki, lakini kufikia sasa haijachukua hatua yoyote ya maana katika kuunga mkono Hamas na makundi mengine ya mapambano ya ukombozi wa Palestina katika ukanda huo. Makundi ya Palestina yanapinga hatua ya Mahmoud Abbas ya kumtambulisha waziri mkuu mpya katika mazingira hayo. Makundi hayo yanasema kwamba hatua ya upande mmoja ya Mahmoud Abbas ya kuunda baraza jipya la mawaziri katika mazingira ya sasa itapelekea kuongezeka fikra za kuhodhi madaraka na kuchochea migawanyiko kati ya Wapalestina.

Mauaji ya kimbari ya Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza

Taarifa iliyotolewa na makundi hayo inasema kuwa kipaumbele muhimu zaidi kwa sasa ni kukabiliana na uchokozi na siasa za mauaji ya kimbari na njaa ambazo utawala wa Kizayuni unazitekeleza dhidi ya watu wa Gaza. Inasema kuchukuliwa maamuzi na mtu mmoja na kuunda serikali mpya bila maridhiano ya kitaifa kunaimarisha siasa za kuhodhi madaraka na wakati huo huo kuzidisha migawanyiko kati ya Wapalestina. Taarifa hiyo inasisitiza upinzani wa makundi ya mapambano ya Palestina dhidi ya sisitizo la Mamlaka ya Ndani ya Palestina la kuendeleza siasa za upande mmoja za kuhodhi madaraka na kuzichukulia hatua kama hizo kuwa ni ishara ya ukubwa wa mgogoro ndani ya uongozi wa mamlaka hiyo na kuwa mbali kwake na ukweli wa masuala pamoja na watu wa Palestina.

Nukta muhimu katika suala hili ni kwamba Mahmoud Abbas, Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amejaribu kupata ridhaa ya Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika uteuzi wake wa waziri mkuu huyo mpya. Kwa hakika hiyo ni moja ya sababu za makundi ya muqawama kupinga kuarifishwa kwa waziri mkuu huyo mpya. Kuhusiana na hilo, vyanzo vya habari vya Palestina vinasema chaguo hilo limefanywa licha ya upinzani ndani ya harakati ya Fat'h yenyewe. Vyanzo hivyo pia vimetangaza wazi kuwa Muhammad Mustafa ni chaguo lililofanywa na Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu.

Waziri mkuu huyo mpya wa Palestina mwenye umri wa miaka 70, ambaye ana shahada ya uzamivu au Phd katika masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha George Washington, ana uzoefu wa miaka 15 ya kufanya kazi katika Benki ya Dunia na amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) tangu 2022. Pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi katika tawala zilizopita za mamlaka hiyo. Kwa kuzingatia historia hiyo, shakhsia huyo anachukuliwa kuwa waziri mkuu mwenye mielekeo ya Magharibi ambaye anaungwa mkono na Marekani.