Mar 22, 2024 02:24 UTC
  • Kuendelea mapambano, mhimili wa muqawama dhidi ya mauaji ya kimbari ya Gaza

Ikiwa ni katika kukabiliana na muendelezo wa mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza, mhimili wa muqawama wa Palestina, Lebanon, Iraq na Yemen umeshambulia maeneo kadhaa ya Wazayuni.

Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, tangu Oktoba 7, 2023, utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia wa kawaida wa Ukanda wa Gaza ambapo kufikia sasa umeua kikatili Wapalestina zaidi ya 32,000.

Katika masaa machache yaliyopita, ndege za kivita na makombora ya utawala huo wa kibaguzi yamelenga nyumba kadhaa katika kitongoji cha Al-Rimal na pambizoni mwa Hospitali ya Al-Shifa, na wakati huo huo Wazayuni kuzuia timu za matibabu kwenda kuwatibu wahanga wa mashambulio katika maeneo hayo.

Idadi kubwa ya familia katika kitongoji cha Al-Rimal magharibi mwa mji wa Gaza ziko chini ya mzingiro kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara utawala ya vikosi vya Israel katika eneo hilo.

Askari wa Kizayuni pia wameushambulia mji wa Khalil na kambi mbili za wakimbizi za Ain al-Sultan na Aqaba Jabr huko Jericho katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika kujibu mashambulio hayo ya Wazayuni, muqawama wa Kiislamu wa Iraq umelenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion ulio katikati ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia ndege isiyo na rubani.

Muqawama wa Iraq ulitangaza Jumatatu asubuhi kwamba umelenga kituo cha ndege zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni katika milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel nchini Syria.

Vikosi vya brigedi ya al-Quds, tawi la kijeshi la harakati ya Jihad Islami ya Palestina, vimetangaza kwamba wapiganaji wake walipambana na baadhi ya wanajeshi wa Kizayuni karibu na jengo la hospitali ya Al-Shifa, ambapo askari kadhaa wa utawala huo waliangamizwa au kujeruhiwa.

Ukatili wa Israel Gaza

Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon (Hizbullah) pia umetangaza kutekeleza operesheni kadhaa dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kujibu jinai unazotekeleza dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza na pia mashambulio ya mara kwa mara unayofanya katika mikoa ya kusini mwa Lebanon, na kutangaza kupitia taarifa kwamba umefanikiwa kuwalenga askari wa Kizayuni katika eneo la muinuko wa al-Taihat, na kuangamiza pamoja na kujeruhi idadi kadhaa miongoni mwao.

Wapiganaji wa muqawama wa Kiislamu pia wamelenga kwa kombora kikosi cha jeshi la Kizayuni kusini mwa kambi ya kijeshi ya Branit.

Maeneo mengine ya jeshi la Kizayuni katika milima inayokaliwa kwa mabavu ya Kafr Shoba na vilevile maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Sheba huko Lebanon pia yamelengwa kwa maroketi.

Katika operesheni nyingine, wapiganaji wa Hizbullah wamelenga maeneo ya kijeshi ya maadui huko Barka Risha na viunga vyake kwa maroketi. Hii ni katika hali ambayo jeshi la Kizayuni kwa mara nyingine limeshambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon vikiwemo vitongoji vya Rabbu Thalahin, al Naqourah na Meiss al-Jabal.

Wakati huo huo gazeti la Haaretz la lugha ya Kiibrania limemnukuu Lucian Leor, mkuu wa Idara ya Afya ya Akili ya jeshi la utawala wa Kizayuni akisema kuwa, takriban wanajeshi 2,000 wa Israel wamekumbwa na matatizo ya kiakili kutokana na vita vya Gaza ambapo wametumwa katika vituo vya mapumziko kwa ajili ya kupata matibabu na huduma za lazima za kiafya.

Pia amesema tangu Oktoba 7, askari wapatao 3,000 wamefanyiwa uchunguzi wa kisaikolojia, ambapo askari wasiopungua 1,700 wamepatikana kuwa na matatizo ya akili yaliyosababishwa na vita.