Mar 30, 2024 06:04 UTC

Televisheni ya CNN ya Marekani imenukuu taarifa ya jeshi la Israel likikiri kuwaua Wapalestina wawili na kufukia miili yao kwa kutumia tingatinga, baada ya televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kurusha hewani kipande cha video kinachoonyesha undani wa mauaji hayo.

Jeshi la Israel limehalalisha mauaji hayo kwa kudai katika taarifa yake kwamba, mauaji ya Wapalestina hao wawili yalitokea baada ya kukaribia eneo la operesheni katikati mwa Gaza kwa njia ya kutia shaka.

Hata hivyo, picha za video zilizonaswa na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar zinaonyesha wanaume wawili wa Kipalestina wasio na silaha, mmoja akipunga hewani kitambaa cheupe mara kwa mara kuashiria kujisalimisha, kabla ya askari katili wa jeshi la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuwapiga risasi na kisha kuzifukia maiti zao kwenye kifusi kwa kutumia tingatinga karibu na mji wa Gaza.

Profesa Richard Falk, Ripota Maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu huko Palestina amesema, ufyatuaji risasi huo uliofanywa na askari wa Kizayuni ni "uthibitisho wa wazi wa kuendelezwa ukatili wa Israel huko Gaza" ambao umekuwa kama "jambo la kila siku".

Bada ya kitendo hicho cha kinyama, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, majanga chungu nzima yaliyowapa watu wa Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi 6 iliyopita ni maabara ya kupima ni kwa kiwango gani nchi na jamii ya kimataifa zinavyoheshimu haki za binadamu.

Kan'ani ameongeza kuwa, msimamo wa nchi na viongozi wa serikali zinazodai kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai mbaya iliyofanywa na askari wa utawala wa kibaguzi wa Israel katika pwani ya kusini magharibi mwa Gaza ya kuwaua na kuwazika vijana wawili wa Kipalestina ambao hawakuwa na silaha, unaonesha ni kwa kiasi gani wanatekeleza kauli mbiu zao na madai ya kutetea haki za binadamu.