Apr 14, 2024 07:50 UTC
  • Biden amwambia Netanyahu kwamba Marekani haitashiriki katika vita vya Israel dhidi ya Iran

Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kwamba Marekani haitashiriki katika mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran.

Duru katika Ikulu ya Rais wa Marekani zimesema kauli hiyo ilitolewa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya Biden na Netanyahu siku ya Jumamosi, kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limefanya mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya maeneo muhimu ya kijeshi ya Israel, kujibu mashambulizi ya kigaidi ya utawala wa Israel ya tarehe 1 Aprili dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Wakati wa mazungumzo hayo, Biden aliweka wazi kuwa Marekani haitahusika katika vitendo vyovyote vya kichokozi dhidi ya Iran na inasemekana Netanyahu ameafiki msimamo huo.

Moja ya makombora ya Iran yaliyotumika kushambulia Israel

Afisa huyo wa White House amesema kuwa Biden na washauri wake wakuu wana wasiwasi mkubwa kwamba iwapo Israel itajibu mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyotekelezwa na Iran basi kutaibuka mgogoro mkubwa zaidi wenye matokeo mabaya.

Biden anatazamiwa kufanya mazungumzo leo Jumapili na viongozi wa kundi la G7  kujadili kile ambacho kimetajwa kuwa "jibu la pamoja la kidiplomasia" kwa operesheni hiyo ya kijeshi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel.