Apr 14, 2024 11:11 UTC

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vinazikanusha picha na mikanda ya video inayosambazwa na vyombo kadhaa vya habari, ikionyesha maeneo tofauti ndani ya utawala huo yaliyolengwa na makombora ya Iran ikiwa ni kufuata na kutekeleza sera ya habari ya baraza la mawaziri la vita la utawala huo haramu.

Siku 10 baada ya shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel lililolenga sehemu ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, ambao unahesabika kuwa sehemu ya ardhi ya Iran na kupelekea kuuawa shahidi washauri saba wa Iran walioko kisheria nchini Syria na kutochukuliwa msimamo wowote wa wazi na jamii ya kimataifa dhidi ya hatua hiyo haramu ya utawala wa Kizayuni, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu usiku wa kuamkia leo Jumapili limerusha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea maeneo ya utawala wa Kizayuni ili kuutia adabu utawala huo kwa jinai uliyofanya.
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, pasi na kuashiria picha na mikanda kadhaa ya video inayoonyesha maeneo tofauti ya kijeshi yaliyolengwa na makombora ya balestiki ya Iran, Halil Rosen, ripota wa Channel 14 ya utawala wa Kizayuni amedai kuwa wimbi la pili la mashambulio yaliyofanywa na Iran ambalo lilikuwa la makombora, halikusababisha madhara yoyote na kwamba kiwango cha uharibifu uliosababishwa ni sifuri.

Kuhusiana na suala hilo, kituo cha habari cha CNN kimenukuu duru ya Marekani ikisema, hakuna uhakika kama mitambo ya ulinzi wa anga ya Marekani itakuwa imefanikiwa kukabiliana na ndege zote hizo zisizo na rubani na makombora yote hayo yaliyorushwa na Iran.

 
Katika mahojiano na Al Jazeera, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Jordan Fayr Al-Dawiri amesema, Israel inajaribu kusema kuwa shambulio hilo la Iran halikufanikiwa na maeneo yaliyolengwa kwa makombora yalipata hasara ndogo tu.
 
Wakati Wazayuni wanajaribu kwa kila njia kuonesha kwamba mitambo yao ya ulinzi wa anga imeweza kuzuia idadi kubwa ya makombora ya Iran, hivi sasa wanakabiliwa na mtihani mkubwa, ambao ni wa mikanda ya video iliyosambazwa na raia wa Palestina, inayoonyesha maeneo yanayoripuliwa na makombora na hivyo kuvipa kibarua kigumu vyombo vya Kizayuni vinavyohusika na ufichaji na ubanaji wa ukweli halisi wa mambo .../