Jul 17, 2023 04:32 UTC
  • Wazayuni wenye misimamo mikali wavamia tena msikiti wa al-Aqswa

Wazayuni maghasibu wenye misimamo ya kufurutu ada Kwa mara nyingine tena wameuvamia msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Duru za Palestina zimetangaza kuwa, idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kuchupa mpaka wameendeleza vitendo vyao vya kichochezi baada ya kuvamia msikiti wa al-Aqswa huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.

Mashuhuda wanasema kuwa, uvamizi wa walowezi hao wenye itikadi kali ulifanyika chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel. 

Hii si mara ya kwanza kwa walowezi wa Kizayuni kuvamia msikiti wa al-Aqswa wakisaidiwa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel.

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.

Tags