Kumbukumbu ya Kuzaliwa Bibi Zaynab al Kubra AS
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) binti ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s); mwanamke ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na fadhila, elimu, subira na ushujaa mkubwa aliokuwa nayo. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab (a.s) hapa nchini imepewa jina la "Siku ya Wauguzi".
Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) alizaliwa tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadul Awwal
 mwaka wa 5 au wa 6 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Mwaka huu 
tunaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab mjukuu wa Mtume saw 
katika hali ambayo haram yake tukufu kwa sasa ina mazingira tofauti 
katika mji wa Damascus nchini Syria. Katika miaka hivi ya karibuni ya 
vita na machafuko huko Syria eneo hilo takatifu mara kadhaa limekabiliwa
 na mashambulio ya makundi ya kitakfiri. Bibi Zaynab (a.s) anayejulikana
 kama Shujaa wa Karbala na mbeba bendera ya harakati baada ya kuuawa 
shahidi ndugu yake yaani Imam Hussein bin Ali (a.s), alizaliwa na 
kulelewa katika nyumba iliyokuwa imejaa huba, fadhila na utukufu yaani 
nyumba ya Bibi Fatima Zahra na Imam Ali bin Abi Twalib (a.s). Bibi 
Zaynab (as) alirithi matukufu yote kutoka kwa baba yake yaani Imam Ali 
(a.s) na mama yake Bibi Fatima (a.s). Akiwa chiniya usimamizi na 
uangalizi wa malezi ya moja kwa moja ya wazazi wake hao watukufu aliweza
 kukwea na kufikia daraja za juu za utukufu, ubora na ukamilifu. Bibi 
Zaynab (a.s) alijifunza upole na uvumilivu kutoka kwa kaka yake Imam 
Hassan (as) huku akijifunza ushujaa kutoka kwa Imam Hussein (as). Ni 
kutokana na sifa hizo bora ndipo ikadhihiri nuru na utukufu wa Kiislamu 
katika haiba ya mwanamke huyo mwema.
Bi Zaynab AS aliondokea kuwa na 
taqwa, subira, kufungamana na maadili mema na sifa nyingine njema ambazo
 alijifunza kutoka kwa mama yake mwema ambaye ni mbora wa wanawake yaani
 Fatima Zahra AS. Bibi Zaynab (as) aliipitisha sehemu ya utoto wake 
kando ya babu yake yaani Mtume SAW na kupitisha moja ya vipindi 
vilivyojaa kumbukumbu nzuri. Hata hivyo kipindi hicho hakikudumu, kwani 
Bwana Mtume SAW aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Aidha haukupita 
muda mrefu, mama yake naye akarejea kwa Mola wake. Licha ya kuwa Bibi 
Fatima Zahra (as) hakupitisha muda mrefu sana akiwa pamoja na watoto 
wake; lakini katika kipindi hicho hicho kifupi alichokuwa nao, 
aliwafunza watoto wake hao somo la juu kabisa la kumuabudu Mwenyezi 
Mungu na kutetea haki. Darsa yake ilijaa hamasa na ikhlasi na mwalimu 
huyo alikuwa akifanya hima kubwa ya kuwafundisha wanawake akhlaqi ya 
Kiislamu kwa mbinu ya kivitendo.
Sayyida Zaynab (as) alikuwa na akili
 ya hali ya juu, kiasi kwamba, katika kipindi hicho hicho cha utoto na 
kuinukia kwake aliweza kuhifadhi kwa moyo hotuba aali na iliyojaa 
madhumuni makubwa ya mama yake katika msikiti wa Mtume SAW yaani Masjdun
 Nabi. Hiyo ilikuwa ishara ya wazi ya upana wa fikra na hali ya kupevuka
 kifikra ya binti huyo aliyekulia katika maktaba ya Wahyi. Kielimu, Bibi
 Zaynab (as) alikuwa amebobea mno kiasi kwamba, umashuhuri wa elimu yake
 uliwafanya wanaume na wanawake wa Bani Hashim wampe lakabu ya "Mwanamke
 Mwenye Hekima."
Kwa hakika Zaynab (as) alikuwa mashuhuri miongoni 
mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio
 la Karbala, Bi Zaynab (as) alisimama kidete na kukabiliana barabara na 
dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza 
malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (as). Wanawake na mabinti wa
 Madina walikuwa wakienda katika nyumba ya Bibi Zaynab kwa ajili ya 
kujifunza elimu na maarifa. Zaynab kwa upande wake alikuwa akiitumia 
fursa hiyo kuwabainisha masuala mbalimbali ya kidini, kijamii na 
kisiasa. Darsa hizo za elimu ziliendelea pia wakati Bi Zaynab alipokuwa 
mjini Kufa baada ya baba yake kuelekea katika mji huo. Katika zama hizo 
wanawake na mabinti waliokuwa na hamu, shauku na raghba ya elimu 
walimtumia ujumbe Imam Ali AS na kumueleza kwamba, tumesikia kwamba, 
binti yako Zaynab kama alivyokuwa mtukufu mama yake, ni chemchemi ya 
elimu na maarifa na ana elimu na ukamilifu; hivyo turuhusu tuje kwake na
 kunufaina na elimu yake.
Bi Zaynab kama walivyo watu wengine wa 
nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW hakuwa nyuma katika masuala ya kiibada,
 dua na kunong'ona na Mwenyezi Mungu. Alitambulika kuwa mchaji Mungu na 
mtu aliyezama katika ibada na uchaji Mungu. Alikuwa akiamka nyakati za 
usiku na kuacha usingizi na kisha kusimama akifanya ibada na 
kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mbali na Swala za usiku alikuwa 
akisoma mno kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani Tukufu. Baada ya 
tukio la Karbala licha ya masaibu, machovu, mateso na taabu 
alizokabiliana nazo yeye pamoja na watu wengine wa familia ya kaka yake 
yaani Imam Hussein (as), katu hakusahau au kughafilika kusali Swala za 
usiku. Imam Sajjad (as) anasimulia akisema: Shangazi yangu Zaynab (as) 
alikuwa akisali Swala zake zote za wajibu na mustahabu tukiwa njiani 
kutoka Kufa tukipelekwa Sham; na baadhi ya wakati alikuwa akitekeleza 
taklifu hizo za kidini akiwa amekaa kutokana na njaa kali na kudhoofika 
mwili."
Sifa nyingine kubwa ya Bi Zaynab AS ni uvumilivu na subira 
isiyo ya kawaida aliyokuwa nayo. Aidha aliondokea kuwa mashuhuri 
kutokana na kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza na inaelezwa kwamba, 
nyumba yake mjini Madina ilikuwa kimbilio la wasio na uwezo na 
waliokwama katika mambo yao.
Mmoja wa watafiti anaandika kuhusiana na
 hali hiyo kwa kusema: "Muamala na radiamali ya Bibi Zaynab (as) dhidi 
ya maadui, ilikuwa ya kushangaza na kustaajabisha. Aliweza kuwahutubu 
kwa maneno makali mno viongozi jeuri, licha ya wao kuwa na madaraka na 
uwezo mkubwa. Kwa sauti ya juu, aliweza kuitikisa kasri ya kidhalimu na 
ghasibu ya Bani Umayya, sanjari na kuifedhehesha majlisi ya Yazid kwa 
maovu yake kupitia hotuba aliyoitoa mbele yake na watu wake wa karibu." 
Aidha miongoni mwa sifa nyingine adimu za Bibi Zaynab (as) ni ushujaa wa
 hali ya juu aliokuwa nao. Mtukufu huyo alisimama kwa nguvu zake zote na
 kupambana na madhalimu na hata kufikia kupewa lakabu ya "Simba wa Bani 
Hashim." Katika majlisi ya Ibn Ziyad, mtawala wa mjini Kufa Iraq, Bibi 
Zainab (as) bila kujali kuwa mtawala huyo aliyekuwa na kila uwezo wa 
kidhahiri, alikuwa amekaa kwenye kasri lake, huku bila kuzingatia 
maswali aliyoyatoa Ibn Ziyad, Bibi Zainab (as) alimdhalilisha mtawala 
huyo na kumwita fasiki na mwovu. Akijibu maneno ya kejeli ya Yazid dhidi
 ya ushujaa wa Bani Hashim, Bibi Zainab alisema: "Nakuona mdogo zaidi ya
 ninavyoweza kukusifia, lakini nifanyeje kwa zama ambazo watu 
wamekengeuka njia ya haki na kukutawalisha wewe juu yao, ukapata uwezo 
wote huu na kuweza kumuua shahidi mjukuu wa Mtume na kuwachukua mateka 
watu wa familia yake..."
Bibi Zainab (as) alishuhudia tukio chungu, 
gumu, la kusikitisha na la kihistoria la Karbala. Wakati alipouawa 
shahidi Imam Hussein na wafuasi wake 72, Bibi Zainab (as) alibeba jukumu
 zito kabisa la tukio hilo. Mbali na hayo alikuwa na jukumu la 
kuwaongoza manusura wa Ahlul-Bayt wa Mtume (saw) kutoka mjini Karbala 
hadi Sham, na kutoka Sham hadi mjini Madina. Licha ya kutokea tukio la 
siku ya Ashura huko Karbala, lakini Bibi Zainab (as) alikabiliana nalo 
kwa msingi wa ridhaa ya Mwenyezi Mungu na tokea kujiri kwa tukio hilo 
hadi kufa kwake, hakulalamikia jambo lolote, bali alisikika akimshukuru 
tu Mola wake. Kwa mfano, siku chache baada ya kujiri mauaji ya Karbalaa,
 akiwa katika kasri la kidhalimu mjini Kufa, Ibn Ziyad alimkejeli Bibi 
Zainab kwa kusema: "Umeona vipi hekima ya Mwenyezi Mungu juu ya 
Ahlul-Bayt?" Mtukufu huyo akamjibu kwa kusema: "Sikuona kitu kingine ila
 uzuri."
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri, baraka na 
fanaka kwa mnsaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Sayyida Zaynab AS binti 
wa Imam Ali bin Abi Talib AS, siku ambayo kama tulivyaoshiria mwanzoni 
mwa kipindi hiki maalum huadhimishwa hapa nchini kama "Siku ya Wauguzi".
 
							 
						 
						