Nchi za Ulaya zakosolewa kwa kupuuza mgogoro wa wahajiri
Bunge la Ulaya limekosoa baadhi ya nchi za bara hilo kwa kupuuza mgogoro wa wahajiri na hivyo kufanya suala hilo kuwa gumu zaidi kulitatua.
Mkuu wa bunge hilo, Martin Schulz amesema kuwa kutowajibika baadhi ya nchi za Ulaya na kufeli viongozi kutekeleza majukumu yao kuhusiana na wahajiri kumelifanya suala hilo kuwa kubwa na kutishia mustakabali wa Umoja wa Ulaya.
Mkuu huyo wa Bunge la Ulaya amesema baadhi ya viongozi walitoa ahadi katika kikao kilichopita cha wakuu wa EU lakini ahadi hizo za kusaidia kutatua kadhia ya wahajiri bado hazijatekelezwa.
Amekumbusha kuwa mgogoro wa wahajiri usipotatuliwa haraka utalitumbukiza bara Ulaya kwenye matatizo makubwa siku za usoni. Amesema usalama wa bara hilo uko mashakani kutokana na kushindwa viongozi kudhibiti wimbi la wahajiri wanaoingia kila siku.