Juhudi za kurejesha amani na uthabiti nchini Mali
Sambamba na kuendelea mivutano na machafuko nchini Mali, Rais wa nchi hiyo ametangaza kuwa, utafanyika mkutano wa maridhiano ya kitaifa wenye lengo la kuhitimisha hitilafu zilizopo katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Akihutubia taifa kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa 2017, Rais Ibrahim Boubacar Keita amesema kuwa, mkutano wa maridhiano ya kitaifa utafanyika nchini humo Machi mwaka huu na kwamba, kipaumbele cha mkutano huo ni kutekelezwa hati ya makubaliano ya amani ambayo ilitiwa saini mwaka 2015.
Rais wa Mali sanjari na kuashiria kwamba, katika mkutano huo kutajadiliwa pia sababu za hitilafu zilizopo hivi sasa ameonesha matumaini aliyonayo kwamba, mkutano huo itakuwa nukta muhimu kwa ajili ya kuhuisha umoja nchini Mali.
Ni kwa muda sasa machafuko yamekuwa yakiendelea kaskazini mwa Mali na makundi ya wanamgambo wenye silaha yamekuwa yakiyadhibiti maeneo hayo tangu mwaka 2012. Kushadidi machafuko katika maeneo hayo hatimaye kuliifanya serikali na makundi ya wanamgambo wa kaskazini mwa nchi hiyo kutiliana saini hati ya makubaliano ya amani Mei mwaka 2015 ikiwa ni natija ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyofanyika nchini Algeria.
Wananchi wa Mali walikuwa na matumaini kwamba, hati hiyo ya makubaliano ingerejesha amani na uthabiti katika eneo linalokabiliwa na hali ya mchafukoge la kaskazini mwa Mali. Hata hivyo makundi ya wanamgambo yalikiuka mara kadhaa usitishaji vita. Katika hali ambayo, pande mbili daima zilikuwa zikisisitiza juu ya kutekelezwa hati hiyo ya makubaliano; lakini kivitendo akthari ya maeneo ya Mali hususan yale ya kaskazini mwa nchi hiyo yangali yanashuhudia mashambulio na mapigano.
Filihali, makundi mbalimbali ya wanamgambo nchini Mali yanaendeleza harakati zao. Harakati ya Ukombozi wa Azawad (MNLA) na wanamgambo wa Tuareg ni miongoni mwa makundi muhimu yanayoendesha vita dhidi ya serikali ya Bamako. Nchi ya Mali kama zilivyo baadhi ya nchi nyingine za eneo hilo la Afrika imekuwa eneo muhimu la harakati za makundi ya kigaidi kutokana na ukosefu wa amani na usalama. Hii ni katika hali ambayo, ni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa mbapo kuna kikosi cha zaidi ya askatri 11,000 wa kusimamamia amani wa Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Mali MINUSMA.
Fauka ya hayo, Rais Francois Hollande wa Ufaransa Januari mwaka 2013 alituma nchini Mali kikosi cha nchi yake kwa madai ya kwenda kupambana na ugaidi. Kikosi cha Ufaransa kilipelekwa kaskazini mwa Mali kwa kisingizio cha kuikomboa miji muhimu ya Kidal, Gao na Timbuktu ambayo ilikaliwa kwa mabavu na makundi ya waasi yenye misimamo mikali ambayo yalikimbilia katika mipaka ya Mali na Niger baada ya kuangushwa serikali ya Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya.
Licha ya hatua kadhaa kuchukuliwa, lakini jeshi la Mali, kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA na wanajeshi wa Ufaransa hawana udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Mali hususan ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika mazingira kama haya inaonekana kuwa, serikali ya Mali imo mbioni kuhakikisha kwamba, vipengee vya hati ya makubaliano baina yake na makundi ya wabeba silaha vinatekelezwa. Ukweli ni kuwa, hadi sasa kumeshafanyika vikao mbalimbali kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la utekelezaji wa hati hiyo ya makubaliano. Hivi sasa viongozi wa Mali wanafuatilia suala la kufanyika mkutano mwingine utakaoyashirikisha makundi yote ya wanamgambo na wapinzani.
Alaa kulli haal, ni lazima kuwa na matumaini kwamba, hitilafu hizo zitapatiwa ufumbuzi katika meza ya mazungumzo; kwani mazungumzo na kuonesha nia njema kwa pande zote mbili ndio njia pekee ya kufikia amani na uthabiti na hivyo kuzuia uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.