Takwimu Jumapili
Leo ni Jumapili tarehe 26 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1437 Hijria sawa na tarehe 6 Machi, 2016 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1157 iliyopita, sawa na tarehe 26 Jamadil Awwal 1437 Hijria, alifariki dunia Ibn Tayfur, mwandishi na malenga wa Kiarabu. Ibn Tayfur alizaliwa mwaka 204 Hijiria. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, alijishughulisha na uandishi wa vitabu mjini Baghdad. Katika kipindi hicho Ibn Tayfur alifahamiana na maulama na wasomi mashuhuri wa mji wa Baghdad. Ni baada ya hapo ndipo Ibn Tayfur akawa mashuhuri katika uwanja wa mashairi. Mbali na uwanja huo, msomi huyo alijulikana sana kwa uandishi wa vitabu mbalimbali ambavyo hii leo vinapatikana katika maktaba za mji wa Baghdad, Iraq.
Siku kama ya leo miaka 541 iliyopita, alizaliwa mjini Caprese Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia. Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake juu ya fani hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika fani hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye, ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512 Miladia. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.
Siku kama ya leo maka 116 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa pikipiki raia wa Ujerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.
Siku kama ya leo, miaka 79 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia. Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege. Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6.
Na siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.