Watu nusu milioni kuongezeka Cairo, Misri mwaka huu
Idadi ya watu katika mji mkuu wa Misri, Cairo, itaongezkea kwa nusu milioni mwaka huu, hili likiwa ni ongezeko kubwa zaidi la idadi ya watu mjini duniani, jambo ambalo limezidisha mashinikizo katika uchumi wa Misri ambao ungali unajaribu kujikwamua kutoka katika mgogoro wa kisiasa wa miaka sita sasa.
"Cairo Kubwa," eneo la mji linalojumuisha Cairo na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Giza na Qalyubia, ni makao ya watu milioni 22.8 na idadi yao itaongezeka kwa nusu milioni mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa ya Euromonitor International, idadi hiyo ya watu milioni 22.8 ni robo ya watu wote milioni 92 nchini Misri.
"Wastani wa ongezeko la watu Misri ni asilimia 2.4 kwa mwaka ambayo ni mara mbili zaidi ya nchi zinazostawi," amesema Mohammad Abdelgalil, mshauri ya shirika la takwimu la CAPMAS.
Uchunguzi umebaini kuwa kutokana na umasikini mkubwa huko kusini mwa Misri, familia hufadhilisha kupata watoto wengi ili wawe chanzo cha pato. Hatimaye watoto hugura na kuelekea katika miji mikubwa kutafuta ajira ambayo haipatikani katika miji yao.
Serikali ya Misri inasema, kuna mitaa 351 ya mabanda nchini humo, aghlabu ya mitaa hiyo ikiwa katika mji mkuu Cairo. Uchumi wa Misri ulistawi kwa asilimia 4.3 mwaka 2015-2016 lakini ustawi huo hautoshi kukidhi mahitaji ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Idadi ya watu Misri inatabiriwa kufika milioni 160 hadi 180 katika kipindi cha miezi 40 ijayo.