Jun 29, 2017 04:10 UTC
  • Kuongezeka changamoto za Saudia Arabia kutokana na siasa zake mbovu

Habari zinaeleza kuongezeka kwa changamoto zinazoikabili Saudi Arabia kutokana na siasa mbovu na za kichokozi zinazotekelezwa na watawala wa nchi hiyo katika eneo.

Mvutano wa kisiasa ambao umechochewa na Aal Soud na washirika wake wa karibu yaani Imarati, Bahrain na Misri dhidi ya Qatar ambayo inafuatilia siasa huru zaidi katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambalo linadhibitiwa na Saudia, umeipelekea nchi hiyo ya kifalme kutengwa katika eneo. Siasa mbovu ambazo zimekuwa zikitekelezwa na watawala wa Riyadh katika miezi ya hivi karibuni zimezua malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wa baraza hilo dhidi ya Saudia. Upinzani wa wazi wa nchi kama vile Omani na  Kuwait  na ukosoaji mkali wa Qatar dhidi ya siasa za ubabe za Wasaudia umepelekea kujitokeza kambi mpya zinazokabiliana miongoni mwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Nchi hizo pinzani zinalichukulia Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Ujemi kuwa chombo kinachotumiwa na Wasaudia kufikia malengo yao bila ya kujali maslahi ya nchi nyingine wanachama na kwa hivyo haziko tayari tena kushirikiana na baraza hilo.

Mfalme Salman wa Saudia  (kulia) akiwa na Amir Tamim bin Hamad wa Qatar

Katika mazingira hayo wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba ni Sudia ndiyo iliyoshindwa katika uchochezi wake wa kisiasa wa hivi karibuni dhidi ya Qatar.

Kwa ujumla, wataalamu hao wanasema kuwa dalili ya wazi zaidi inayothibitisha kwamba Saudia imetengwa kieneo katika mgogoro wake wa hivi sasa ambapo imetoa masharti yasiyo ya kimantiki na yasiyokubalika dhidi ya nchi hiyo ndogo ya Kiarabu ni kuwa imepoteza marafiki wake kadhaa katika eneo. Katika upeo wa kimataifa pia watawala wa Saudia wametengwa kutokana na siasa zao mbovu za kuendelea kuyaunga mkono kifedha na kwa silaha makundi tofauti ya kigaidi yanayofanya uharibifu na kutekeleza mauaji ya kutisha kineo na kimataifa. Hii ni katika hali ambayo hatua ya watawala wa Riyadh ya kufuata kibubusa siasa za Marekani na kuimwagia mapesa kwa lengo la kuiridhisha ili iwaunge mkono katika kila wanalolifanya na vilevile malumbano ya kuwania madaraka yanayoonekana katika ukoo unaotawala nchini humo ni suala ambalo limewaletea matatizo mengi.

 Rais Trump na Mfalme Salman wakitiliana saini  mkataba wa mamia ya mabilioni ya dola

Siasa hizo zimewafanya watawala hao wazidi kuwategemea Wamarekani na hivyo kuwa vibaraka wao wakubwa. Siasa hizo zilionekana wazi hivi karibuni ambapo Mfalme Salma wa Saudia na mtoto wake Muhammad bin Salman waliamua kumumwagia Rais Donald Trump wa Marekani mamia ya mabilioni ya dola ili kupata uungaji mkono wake katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Bila shaka tabia hiyo ya Wasaudia imepunguza pakubwa itibari ya nchi hiyo katika ngazi za kimataifa. Isitoshe tabia hiyo pia imekuwa na matokeo mabaya ndani ya nchi ambapo siasa zao za ukandamizaji na kuhodhi madaraka zimezua mvutano mkubwa nchini humo. Ukandamizaji wa wanaharakati wa kisiasa na kubanwa uhuru wa raia wa Saudia kumezua malalamiko mengi katika fikra za waliowengi nchini humo. Hii ndio maana katika miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia maandamano ya wananchi wa nchi hiyo wakiwemo Mashia wakitaka  kuheshimiwa haki zao za msingi.

Wasaudia wakiandamana kupinga ukandamizaji na ukatili unaofanywa na watawala wa nchi hiyo

Pamoja na kuwa maandamano hayo yamekuwa ya amani lakini yamekuwa yakikabiliwa na mkono wa chuma wa watawala wasioheshima haki za binadamu wa nchi hiyo. Licha ya ukandamizaji huo lakini wananhi wa nchi hiyo hawajaacha kufuatilia haki zao hizo na wameamua kuzifuatilia kwa nguvu zao zote kupitia jumuiya na makundi tofauti ya kisiasa. Hivi kaibuni kundi moja la siasa la Saudia lilitoa taarifa likitangaza kubuniwa kwake kwa ajili ya kufuatilia kwa amani haki za Wasaudia zinazoendelea kukanyagwa na watawala vibaraka wa nchi hiyo. Matukio ya Saudia yanaonyesha kuwa nchi hiyo inayotawaliwa na ukoo mbovu na unaokandamiza raia wake wa Aal Soud inakabiliwa na migogoro mingi mikubwa ambayo inaendelea kuiharibia itibari ya kimataifa.

Tags