Matamshi ya Trump kuhusu uavyaji mimba wazua utata Marekani
Matamshi ya mgombea anayeoongoza wa chama cha Republican katika mashindano ya kuwania kiti cha rais wa Marekani kuhusiana na uavyaji mimba yamezua mjadala na utata nchini humo. Akizungumza hivi karibuni na televisheni ya MSNBC Donald Trump amesema kuwa wanawake wanaoavya mimba kinyume cha sheria za nchi hiyo wanapasa kuadhibiwa.
Licha ya mahakama kuu ya Marekani kutoa hukumu ya kihistoria miaka 40 iliyopita kuhusiana na suala la uavyaji mimba, lakini bado suala hilo lina waungaji mkono na wapinzani sugu nchini humo. Kundi linalojinadi kuwa ni la watetezi wa uhai nchini humo linasisitiza juu ya haki ya kijusi kuendelea kuwa na hai kwenye tumbo la mama yake na kutaka uavyaji mimba udhibitiwe zaidi. Hii ni katika hali ambayo kundi jingine linalojiita kuwa ni la watetetzi wa haki ya kuchagua, linadai kuwa mama mjamzito ana haki ya kuchagua kati ya kuavya au kuendelea kubeba mimba hadi atakapojifungua. Hata hivyo makundi mawili hayo yanabainisha na kukubaliana juu ya hali maalumu ambapo mama mjamzito anaweza kuavya au kulazimika kubeba mimba hadi wakati wa kujifungua. Kwa mfano kundi la kutetea uhai linasema kuwa mwanamke mjamzito anaruhusiwa kuavya mimba iwapo maisha yake yatakuwa hatarini kutokana na mimba aliyobeba, kubeba tumboni kijusi kilicho na kasoro za kimaumbile, mimba iliyotokana na kubakwa au kufanya zina na mtu wa familia. wafuasi wa haki ya kuchagua pia wamekubali kwamba kuavya mimba baada ya miezi mitatu ya ujauzito hakukubaliki kisheria isipokuwa kwa amri na ushauri wa daktari. Pamoja na hayo mtu kuzungumzia suala tata la kuadhibiwa akina mama wanaoavya mimba kinyume cha sheria nchini Marekani ni jambo ambalo lilikuwa halijawahi kushuhudiwa. Mambo ambayo yamekuwa yakijadiliwa katika uwanja huo ni kuadhibiwa madaktari na zahanati zinazojihusisha na uavyaji mimba kwa kutumia bajeti ya serikali au madaktari wanaojihusisha na jambo hilo kinyume cha sheria. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo matamshi ya Trump ya kuadhibiwa wanawake wanaoavya mimba yakalipua mjadala mkubwa katika vyombo vya habari vya nchi hiyo. Si hayo tu bali Trump ambaye bila shaka haungwi mkono na wengi katika chama chake cha Republican ana misimamo ya kupindukia na inayowachukiza raia wengi wa nchi hiyo kuhusiana na masuala kama vile ya kuzuiwa kuingia nchini Marekani Waislamu na kufukuzwa kwa umati wahajiri wasio halali. Hata hivyo kuhusiana na suala la uavyaji mimba Trump amelazimika kusahihisha matamshi yake aliyokuwa ameyatoa awali kutokana na radiamali kali ya wananchi na hasa wanawake wa Marekani. Amebadilisha matamshi yake ya awali kwamba wanawake wajawazito wanaojihusisha na uavyaji mimba wanapasa kuadhibiwa na badala yake kusema kuwa watu wote wanaohusika na jambo hilo kinyume cha sheria ndio watakaoadhibiwa, akikusudia madaktari na zahanati husika. Hii ni pamoja na kuwa kambi ya kampeni za uchaguzi ya Trump imesema kuwa serikali za majimbo ya Marekani pia zitakuwa na kauli ya kuzingatiwa kuhusiana na suala zima la uavyaji mimba. Pamoja na hayo, inaonekana wazi kwamba Trump yuko kwenye mkondo wa kukwaruzana na kupingwa vikali na wanawake pamoja na mirengo ya uleberali nchini Marekani.