Malalamiko ya wananchi wa Zimbabwe kuhusu siasa za Rais Robert Mugabe
Wananchi wa Zimbabwe wamefanya maandamano kulalamikia siasa za Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.
Karibu wafuasi elfu mbili wa chama cha upinzani cha MDC cha Morgan Tsvangirai wamefanya maandamano mjini Harare kulalamikia siasa za Rais Robert Mugabe. Akizungumza mbele ya wafuasi wake Tsvangirai amesisitiza kuwa, Mugabe ameshindwa kutatua mgogoro wa nchi hiyo na kwamba wananchi wa Zimbabwe wanaamini kuwa, serikali yake haina njia nyingine ila kuporomoka tu. Robert Mugabe ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 92, amekuwa rais wa Zimbabwe tangu mwaka 1980. Hali yake tete ya kiafya imepelekea kuzuka maneno mengi kuhusu mtu wa kurithi kiti chake. Kumekuwa na dhana kuwa, Mugabe anafanya mpango wa kumrithisha kiti hicho mkewe, Grace Mugabe. Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Machi, Mugabe alikanusha uvumi huo na kusisitiza kuwa, rais ajaye wa Zimbabwe lazima achaguliwe kwa njia za kidemokrasia. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, matamshi hayo ya Mugabe yanaashiria azma yake ya kuendelea kuwa rais wa Zimbabwe hadi mwisho wa maisha yake. Katika hali ambayo duru za kisiasa za nchi hiyo zinafuatilia kwa karibu sana hali ya kiafya ya Mugabe, baadhi ya duru hizo zinaamini kuwa, hatua ya Mugabe ya kushindwa kuainisha mrithi wake itazidi kuitumbukiza katika mgogoro nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Hivi sasa hali ya kiuchumi ya Zimbabwe ni ya mgogoro kiasi kwamba baadhi ya ripoti zinaonesha kuwa Zimbabwe ndiyo nchi maskini zaidi barani Afrika hivi sasa. Madhara ya hali mbaya ya hewa maarufu kwa jina la Elnino na miaka miwili mfululizo ya ukame imeifanya Zimbabwe ikumbwe na upungufu mkubwa wa chakula kadiri kwamba hivi sasa kati ya watu milioni tatu hadi nne wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya dharura ya chakula. Wakosoaji wa siasa za Mugabe wanasema kuwa rais huyo amefeli katika siasa zake za kuwapa wenyeji mashamba yaliyokuwa yamehodhiwa na Wazungu. Wanasema kuwa, siasa hizo zimepelekea kupungua sana mazao ya kilimo kama vile mahindi. Ikumbukwe kuwa mwaka 2000 Rais Mugabe alianza kutekeleza siasa za marekebisho ya ardhi akisema kuwa, Wazungu walio wachache wamehodhi sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba ya nchi hiyo na kuwanyima wenyeji haki yao ya kufaidika na neema na rasilimali za nchi yao. Hata hivyo siasa hizo zilizikasirisha nchi za Ulaya na Marekani na kuamua kuiwekea Zimbabwe mashinikizo ya kila namna, sambamba na kushindwa serikali ya Rais Robert kuweka serikali nzuri za kufanikisha siasa hizo. Aidha watu wengi waliokabidhiwa ardhi hizo hawakuwa na uzoefu wa kilimo, serikali ilishindwa kuwadhaminia vyanzo vinavyotakiwa vya fedha na bidhaa zilizozalishwa zilikosa soko; yote hayo yamechangia kuporoka sekta ya kilimo na kuifanya Zimbabwe ikumbwe na upungufu mkubwa wa chakula. Fauka ya hayo hivi karibuni Joice Mujuru, Makamu wa zamani wa Rais wa Zimbabwe ameanzisha chama chake kipya kinachojulikana kwa jina la Wananchi Kwanza. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuanzishwa chama hicho kipya kilichojimegua kutoka katika chama tawala cha Zanu-PF ni ishara mbaya kwa Rais Mugabe na chama chake. Wachambuzi hao wanatabiri kuweko ushindani mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018. Tukirejea katika maandamano ya wafuasi wa chama cha MDC cha Morgan Tsvangirai, weledi wa mambo wanaamini kuwa, uchaguzi mkuu ujao wa nchini Zimbabwe utakuwa na mchuano mkali, na kwamba chama tawala cha Zanu-PF kitakuwa na wakati mgumu sana katika uchaguzi mkuu ujao.