Oct 08, 2019 03:17 UTC
  • Kushirikiana Marekani na Ulaya kuiwekea mashinikizo Uturuki baada ya kugundua gesi

Uhusiano wa Uturuki na Marekani hasa baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 15 Julai 2016, umeendelea kugubikwa na mizozo mingi.

Kinyume na matarajio ya viongozi wa Uturuki juu ya kuboreka uhusiano ya nchi mbili baada ya kuingia madarakani Donald Trump huko Marekani, kivitendo nchi hizo zimeingia katika mizozo mikubwa baina yao. Katika hatua yake mpya kabisa Washington imetangaza kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuiwekea mashinikizo Ankara, kufuatia hatua za serikali ya Uturuki ya kutafuta na kugundua gesi upande wa mashariki mwa Bahari ya Mediterrania. Siku ya Jumamosi, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akiwa nchini Ugiriki na akizungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kyriakos Mitsotakis, aliionya Uturuki na kudai kuwa harakati zake za kutafuta gesi ni kinyume cha sheria na hazikubali. Alisema: "Kuna sheria inayotumika katika uwanja wa kufanya uchunguzi wa nishati ndani ya bahari ya Mediterrania, ambapo kwa mujibu wake, Uturuki haitakiwi iendelee na uchimbaji usiozingatia sheria. Tumekwishaiambia Uturuki kwamba uchimbaji huo, ni kinyume cha sheria na haukubaliki. Sisi pia tutaendeleza njia za kidiplomasia kukabiliana na Uturuki katika jambo hilo." 

Meli ya uchimbaji mafuta ya Uturuki

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameashiria tofauti kali zilizopo kati ya Ulaya na Uturuki katika uwanja huo na kusisitiza kuwa, hakuna nchi inayoweza kuifanya Ulaya Mateka. Uturuki ilianza kuchimba mafuta na gesi karibu na maeneo yasiyo ya makazi ya Cyprus, tangu mwishoni mwa mwezi Februari 2019. Hatua hiyo imepelekea kuongezeka mizozo na nchi majirani, yaani Cyprus na Ugiriki, sambamba na kushuhudiwa pia radiamali ya Umoja wa Ulaya. Kitendo cha serikali ya Ankara cha kutuma meli ya uchimbaji mafuta katika maji ya bahari ya Mediterrania karibu na eneo lisilo na makazi la Cyprus, kilishadidisha mzozo kati ya Nicosia na Ankara, juu ya suala la uchimbaji huo ndani ya bahari. Kabla ya hapo pia Cyprus ilikabidhi shughuli ya uchimbaji mafuta na gesi katika eneo hilo kwa mashirika ya Ufaransa na Italia. Kwa kuzingatia kuwa serikali ya Nicosia ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya, umoja huo ulitoa kauli kali dhidi ya Uturuki. Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, na mwishoni mwa kikao chao, viongozi wa Umoja wa Ulaya walitoa taarifa mjini Brussels wakisisitiza kuwa, uchimbaji mafuta na gesi unaofanywa na Uturuki katika eneo la Cyprus, si halali kama ambavyo pia walilaani vikali kitendo hicho. Uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uturuki umekuwa na mivutano mingi tangu kulipojiri mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli hapo tarehe 15 Julai 2016. Hivi sasa kuna orodha ndefu ya tofauti na mizozo kati ya EU na Uturuki ambayo inaanzia kwenye suala la kusimamishwa mchakato kujiunga serikali ya Ankara katika umoja huo, hadi kufikia kwenye ukosoaji mkali wa Brussels juu ya siasa za ndani na matukio yanayohusiana na mabadiliko ya kiutawala ya nchi hiyo kutoka kwenye mfumo wa kibunge na kuwa mfumo wa urais.

Ugiriki nayo imesimama upande wa Cyprus katika mzozo huo

Kwa kuzingatia kuwa Ugiriki na Cyprus, wanachama wa Umoja wa Ulaya, zina mzozo na Uturuki kuhusiana na suala zima la utafiti na uchimbaji wa gesi baharini, ndio maana serikali ya Brussels nayo ikaamua kusimama na nchi hizo wanachama wa EU dhidi ya Ankara. Kabla ya hapo pia, Umoja wa Ulaya na kufuatia mashinikizo ya Ugiriki na Cyprus, ulitoa taarifa iliyoitaja hatua ya Uturuki kuwa isiyo halali sambamba na kuitahadharisha Ankara kuwa, kama haitakuwa tayari kusitisha shughuli zake za uchimbaji gesi na mafuta, basi utatoa radiamali stahiki dhidi yake. Hivi sasa ambapo Marekani ina mizozo mingi na Uturuki ikiwa ni pamoja na mzozo wa Wakurdi huko kaskazini mwa Syria, hatua ya Ankara ya kununua ngao ya makombora ya S-400 kutoka Russia na hatua ya Ankra ya kuendeleza miamala ya kibiashara na kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Washington inaona imepata nafasi nzuri ya kuibana serikali ya Ankara. Katika uwanja huo Washington inashirikiana na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Uturuki. Pamoja na hayo viongozi wa Ankara hawapo tayari kurudi nyuma hata kidogo kuhusiana na kuendeleza shughuli ya utafiti na kustafidi na nishati katika maeneo ya Cyprus. Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alisema: "Uturuki  inayo haki ya kustafidi na vyanzo vya nishati mashariki mwa Bahari ya Mediterrania sawa na nchi nyingine zilizoko katika mwambao na eneo hilo, ikiwemo Uturuki na Cyprus Kaskazini. Kulindwa haki hiyo ya kimataifa ni moja ya majukumu makuu ya Uturuki kama moja ya nchi washiriki." Kwa kuzingatia hilo inatazamiwa kuwa katika siku zijazo kutashuhudiwa makabiliano zaidi kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kuhusu suala hilo.

Tags