Jumapili, 09 Aprili, 2023
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i96044-jumapili_09_aprili_2023
Leo ni Jumapili tarehe 18 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria mwafaka na tarehe 9 Aprili 2023 Miladia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2023 22:44 UTC
  • Jumapili, 09 Aprili, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 18 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria mwafaka na tarehe 9 Aprili 2023 Miladia.

Miaka 148 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 17 Ramadhani, Mirza Abdul Adhim Khan Qarib mwanafasihi na mhakiki mahiri wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Gorgan, moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi, Abdul Adhim Khan Qarib alikamilisha pia masomo ya nahw, sarf, mantiki, hisabati na fasihi na kuondokea kuwa mwalimu katika taaluma ya fasihi. Ustadh Abdul Adhim Khan Qarib ameandika vitabu mbalimbali kwa ajili ya kuitambulisha lugha ya Kifarsi na fasihi yake. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Qawaid Farsi, Bidayat al-Adab na Qawaid al-Adab. ***

Mirza Abdul Adhim Khan Qarib

 

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama. ***

Mauaji ya kinyama ya Wazayuni katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas

 

Miaka 31 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade. Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao. Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi. ***

Slobodan Milosevic

 

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, iliyosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran ikaingia katika orodha na kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.  Siku hii inafahamika katika kalenda ya Iran kwa jina la "Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia.***

Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia