Jun 27, 2016 04:30 UTC
  • Nchi kadhaa za Ulaya zapinga vitendo vya kunyongwa wapinzani Saudia

Wawakilishi wa nchi za Ufaransa na Ireland katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wamesema kuwa idadi ya watu walionyongwa nchini Saudi Arabia katika mwaka uliopita wa 2015 ni maafa makubwa.

Mwakilishi wa Ufaransa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Elisabeth Laurin amesema kuwa, kiwango kikubwa cha watu walionyongwa nchini Saudi Arabia mwaka uliopita wa 2015 kinaakisi hali ya maafa na ya kusikitisha sana. Laurin amewataka viongozi wa Saudia kukomesha adhabu ya kuwanyonga wapinzani wa utawala wa Aal Saud.

Katika upande mwingine, mwakilishi wa Ireland katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa pia amezungumzia ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaonyongwa nchini Saudi Arabia na kuitaka serikali ya Riyadh kukomesha mwenendo huo.

Ripoti zinasema kuwa, kwa sasa watu 50 wanakabiliwa na hatari ya kunyongwa nchini Saudi Arabia kutokana na kuukosoa au kuupinga utawala wa kifalme wa nchi hiyo.

Hata hivyo na licha ya upinzani wa nchi nyingi dhidi ya hukumu za kunyongwa idadi kubwa ya watu hususan wapinzani wa serikali nchini Saudi Arabia, Marekani na baadhi ya washirika wake wa Magharibi daima wamekuwa wakiitetea na kuihami kwa kila namna serikali ya kifalme ya nchi hiyo.

Tags