Upinzani wa serikali ya Sana'a dhidi ya kutawaliwa nchi hiyo.
Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema katika hotuba yake mbele ya familia za mashahidi wa Yemen kuwa nchi hiyo haitakubali kuwa chini ya udhibiti wa nchi yoyote ya kigeni.
Takriban miaka 9 imepita tangu kuanza vita vya Saudia dhidi ya Yemen, ambapo lengo kuu la Saudi Arabia lilikuwa ni kuiweka madarakani serikali ambayo ingekuwa chini ya udhibiti na matakwa ya serikali ya Riyadh. Kwa upande mwingine, Ansarullah na washirika wake kwa kufuata njia ya muqawama na mapambano walifikisha ujumbe kwamba Yemen ni nchi huru ambayo haitadhibitiwa au kutawaliwa na nchi nyingine yoyote.
Wakati wa vita hivyo, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Marekani ziliteka baadhi ya maeneo ya kusini mwa Yemen, jambo ambalo lilisababishwa na udhaifu na utegemezi wa serikali ya wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na Abd Rabbu Mansour Hadi. Hata hivyo, hakuna sehemu yoyote ya kaskazini mwa Yemen, ambayo iko chini ya udhibiti wa Ansarullah na washirika wake, iliyotekwa ua kukaliwa kwa mabavu na nchi za kigeni. Katika mazungumzo na Saudi Arabia, Ansarullah imetaka kuondoka kusini mwa Yemen vikosi vyote vya kigeni.
Inaonekana kuwa moja ya sababu za kushindwa mazungumzo katika kipindi cha miezi 6 iliyopita ni suala hilo, hasa kwa kuzingatia kuwa Marekani pia kama nchi ya kigeni ina majeshi katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Yemen. Mahdi Al-Mashat awali alisema kuwa Marekani inazuia kufikiwa makubaliano ya amani kwa sababu ya kuendeleza siasa zake za kikoloni nchini humo. Siasa zote zinazotekelezwa katika maeneo yanayodhibitiwa na nchi za kigeni zinakwenda sambamba na sera za Marekani za kujitanua katika maeneo hayo.
Marekani inajaribu kuimarisha siasa zake za kujitanua na kikoloni kupitia mamluki wake walioko kusini mwa Yemen. Kuhusiana na hilo, Wamarekani wanatekeleza njama zao kwa kisingizio cha kutoa mafunzo kwa jeshi la Yemen. Wanajeshi wa Marekani pia wanadai kutoa mafunzo kwa vikosi vya majini vya Yemeni kwenye pwani ya magharibi ya nchi hiyo.
Licha ya tofauti za kiutendaji zilizopo kati ya Ansarullah na baadhi ya makundi mengine ya Yemen, lakini tofauti muhimu zaidi ni sisitizo la Ansarallah juu ya kujitawala Yemen na kuondoka nchi za kigeni kaskazini na kusini mwa nchi hiyo. Mapema, Mohammad Al-Atafi, Waziri wa Ulinzi katika serikali ya Sana'a, wakati akitembelea vikosi vilivyoko eneo la 5 la kijeshi katika maeneo ya al-Tahita, al-Fazah, al-Haima Sahi na al-Jarhari huko katika Pwani ya Magharibi, alitangaza kumalizika kipindi cha kutawaliwa Yemen. Mohammad Al-Bakhiti, mjumbe katika ofisi ya kisiasa ya Ansarullah, awali pia alisema kuwa Wayemen kamwe hawatakubali nchi yao kuwa chini ya udhibiti wa Saudi Arabia au nchi nyingine yoyote na kwamba kipindi cha kutawaliwa kimepita.
Nukta muhimu ni kwamba wananchi wa Yemen wanaunga mkono msimamo wa serikali ya Sana'a na wanasisitiza juu ya uhuru wa nchi yao. Jambo hilo linatiwa nguvu na idadi ya mashahidi ambao ni zaidi 100,000 katika kipindi cha miaka 9 ya vita. Idadi hii ya mashahidi inaonyesha lengo lao thabiti la kulinda na kutetea uhuru wa nchi yao.