Operesheni ya Hamas sawa na vita vya siku 33
Jambo ambalo kwa miezi mingi limekuwa jinamizi kwa jeshi la utawala ghasibu wa Isreal na hasa walowezi wa Kizayuni wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu karibu na mpaka wa Ukanda wa Gaza limetimia kivitendo kufuatia operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha al-Aqsa iliyotekelezwa kwa mafanikio makubwa Jumamosi na wapiganaji shupavu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Operesheni hiyo ya kijeshi, ambayo ilifanywa kwa wakati mmoja kutokea ardhini, angani na baharini sambamba na Hamas kurusha makombora 5,000 kuelekea maeneo yaliyokusudiwa ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, wapiganaji wa harakati hiyo ya mapambano pia waliweza kupenya katika maeneo yanayokaliwa na utawala huo tangu 1948 na kushambulia pamoja na kuteka idadi kubwa ya askari jeshi wa utawala huo vamizi.
Operesheni kama hiyo ya Kimbunge cha Al-Aqsa, ilikuwa haijawahi kushuhudiwa tena katika ardhi hizo na inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika historia ya operesheni za kujitetea Wapalestina dhidi ya hujuma za mara kwa mara za askari na walowezi wa Kizayuni katika ardhi hizo.
Kwa hakika, kile ambacho Hizbullah ilikuwa ikitishia nacho utawala wa Kizayuni, yaani kufanya operesheni ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Hamas imekitekeleza kivitendo na badala ya kaskazini, mashambulizi hayo yametokea kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hii ina maana kwamba vikosi vya Wanamuqawama vinaweza kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu kutokea kaskazini na kusini kwa wakati mmoja na kukutana katika maeneo ya katikati mwa ardhi hizo zilizoghusubiwa.
Hamas na vikosi vingine vya Muqawama wamekuwa wakionya kwamba hawatanyamazia mashambulizi yanayoongezeka kila uchao ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa, kama ambavyo huko nyuma walithibitisha onyo hilo kupitia operesheni ya Upanga wa Quds waliyotekeleza katika uwanja huo.
Kwa operesheni hii ya karibuni, Hamas si tu kwamba imetoa jibu kali kwa mashambulizi yanayoongezeka kila siku ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa, bali pia imelipiza kisasi cha mashambulizi ya kichokozi yanayofanywa na Wazayuni huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Operesheni hii ni jibu la mashambulio, ukandamizaji na mauaji ambayo utawala wa Kizayuni umekuwa ukiyatekeleza dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tokea kubuniwa serikali ya Netanyahu yenye misimamo mikali ya kigaidi na ingawa Gaza kwa kiasi fulani haikukumbwa na mashambulizi hayo, lakini kupitia operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, imeonyesha kuwa inayapa kipaumbele matukio ya Ukingo wa Magharibi, hasa huko Quds Tukufu, inazingatia matakwa ya Wapalestina na kutumia nguvu zake zote za kijeshi na kiulinzi kwa njia nzuri kabisa.
Kwa operesheni hiyo, kushindwa tena kihistoria utawala wa Kizayuni na Netanyahu binafsi, kumeongeza jumla ya vipigo vya Wapalestina kwa utawala huo, na kuna uwezekano kuwa moja ya taathira na matokeo yake itakuwa ni kuporomoka serikali ya muungano ya Netanyahu. Hii ni kwa sababu walowezi wamepata pigo na fedheha kubwa zaidi tangu kuasisiwa kinyume cha sheria utawala wao huko Palestina, na hivi sasa Netanyahu hana chuaguo jingine linaloweza kumfaa katika mazingira ya sasa, na iwapo atachukua njia ya kijeshi bila shaka matokeo yake yatakuwa mabaya zaidi kuliko yale yaliyotokana na operesheni ya Jumamosi ya Kimbunga cha Al-Aqsa.