Je, Ukingo wa Magharibi utaisaidia Gaza?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103376-je_ukingo_wa_magharibi_utaisaidia_gaza
Huku siku chache zikiwa zimepita tangu kuanza operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha al-Aqsa, utawala ghasibu wa Israel umeshadidisha mashambulizi ya kipofu kwenye maeneo ya makazi ya raia huko katika Ukanda wa Gaza ili kujaribu kufidia kipigo ulichopata kutoka kwa wapiganaji wa Hamas.
(last modified 2024-05-29T07:24:47+00:00 )
Oct 12, 2023 03:51 UTC
  • Je, Ukingo wa Magharibi utaisaidia Gaza?

Huku siku chache zikiwa zimepita tangu kuanza operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha al-Aqsa, utawala ghasibu wa Israel umeshadidisha mashambulizi ya kipofu kwenye maeneo ya makazi ya raia huko katika Ukanda wa Gaza ili kujaribu kufidia kipigo ulichopata kutoka kwa wapiganaji wa Hamas.

Utawala huo wa kigaidi umeua na kujeruhi maelfu ya raia wa kawaida na wasio na hatia wa Palestina na hasa watoto wachanga na wanawake, kwa ajili tu ya kujaribu kufidia na kufunika aibu kubwa uliyopata kutokana na kufedheheshwa kijeshi na wapiganaji wa Hamas kupitia operesheni yao ya Kimbunga cha al-Aqsa hivi karibuni. Mbali na hayo unatekeleza mzingiro wa kinyama na kijinai dhidi ya Ukanda wa Gaza ambapo umekata maji, umeme na kuzuia chakula kuwafikia zaidi ya wakaazi milioni mbili wa ukanda huo. Jinai zote hizo ambazo bila shaka ni uhalifu wa kivita, zinatekelezwa kinyume kabisa na kanuni na sheria za kimataifa.

Kufuatia mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni, karibu wakaazi elfu tano wa Ghaza wameuawa shahidi au kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida hasa watoto na wanawake, na kufikia sasa hakuna sura zozote maalumu za wanachama wa Hamas au makundi mengine ya muqawama zinazoonekana kati ya wahanga hao waliouawa shahidi. Dalili kuu ya hilo ni kuwa wengi wa wapiganaji hao ima wako mstari wa mbele wa vita katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa, au wako nyuma ya mstari huo kwa ajili ya kutoa misaada ya dharura na wako tayari kabisa kukabiliana na adui Mzayuni.

Mashambulio makali ya Israel kwenye makazi ya raia

Kwa hivyo, kama kuna rekodi yoyote ambayo imewekwa na utawala wa Kizayuni katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, ni kwamba umeweza kuongeza idadi ya Wapalestina waliojeruhiwa na kufikia zaidi ya 4,000 kupitia mashambulizi makubwa zaidi ya urushaji mabomu katika maeneo ya raia, ambapo katika kipindi cha siku tatu pekee umemwaga tani elfu moja za mabomu kwenye vichwa vya Wapalestina na hivyo kupindukia idadi ya Wazayuni waliojeruhiwa. Wakati huo huo unajaribu kuongeza idadi ya vifo vya Wapalestina ili izidi ya Wazayuni walioangamizwa kwenye operesheni hiyo. Pamoja na hayo, utawala wa Kizayuni haujaweza kumkamata hata mpiganaji mmoja wa Hamas hadi sasa, katika hali ambayo Hamas imewakamata askari vamizi wa Kizayuni zaidi ya 150 na hivyo kusajili mafanikio na ushindi mkubwa zaidi katika historia ya miaka 75 ya utawala wa Kizayuni unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Majeshi yote ya Waarabu hayakuweza kufikia mafanikio kama hayo katika vita vyao vyote na Wazayuni.

Kuendelea mwenendo huo kunaweza kusababisha kuongezeka na kuenea vita hadi nje ya mipaka ya Gaza. Hii ni kwa sababu kabla ya hapo, makundi ya muqawama, ikiwemo Hizbullah, yalikuwa yametishia kwamba hayatanyamaza kimya iwapo Wazayuni wataanzisha mashambulizi ya nchi kavu huko Gaza na kwamba yataingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu kutokea kaskazini. Karibuni yamethibitisha kivitendo kuwa hizo hazijakuwa nara tupu tu bali yako tayari kutekeleza maonyo yao dhidi ya maghasibu hao. Maonyo hayo ni moja ya mambo ambayo yameufanya utawala huo usite kuanzisha mashambulio ya nchi kavu dhidi ya Gaza licha ya kutangaza hali ya vita na kuwarejesha jeshini askari wastaafu. Suala jingine ni kwamba baadhi ya makundi ya muqawama yaliyopo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kama vile Arin al-Usud, tayari yametangaza mshikamano wao na makundi ya mapambano huko Gaza na kusisitiza hadharani kuwa yako tayari kushiriki katika operesheni ya al-Aqsa.

Katika hali hiyo, iwapo makundi hayo yataona kuwa utawala wa Kizayuni umeogopa kuanzisha mashambulizi makubwa ya nchi kavu dhidi ya Gaza na badala yake kuamua kuwaua kiholela raia wa kawaida katika ukanda huo kwa madhumuni ya kuongeza kila siku idadi ya wafu na majeruhi wa Palestina, bila shaka yatachukua hatua ya kukabiliana na watenda jinai hao wa Kizayuni.

Watoto ndio wahanga wakuu wa hujuma ya Israel katika makazi ya raia

Kwa msingi huo, kuna uwezekano wa kutokea operesheni yoyote mpya katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kwa sababu kila mara wananchi na makundi ya muqawama ya Gaza yanapoona kuwa utawala wa Kizayuni unawabana wakaazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuzidisha hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa, huchukua hatua mara moja kwa ajili ya kupunguza mashinikizo na mzigo mkubwa kutoka mabegani kwao. Kwa kutilia maanani kwamba sasa mashinikizo na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yameelekezwa Gaza, ni jambo la kawaida kabisa kutarajia kuwa sasa wakati umefikwa kwa watu na makundi ya muqawama ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nayo kufanya hivyo hivyo, yaani yachukue hatua ya kuwasaidia wenzao wa Gaza ambao wanakabiliwa na mashambulio ya kinyama na kijinai ya utawala ghasibu wa Israel, unaopata uungaji mkono wa pande zote kutoka nchi za Magharibi.