Watu waliozingirwa Gaza wanasubiri msaada wa kimataifa
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika hotuba yake kwenye Kikao cha Amani cha Cairo: 'Tunakutana katikati ya eneo ambalo lina maumivu makali na limesimama hatua moja kutoka kwenye shimo refu. Eneo ambalo hauwezi kukosa kuhuzunika na kukereka na moyo kuuma na kusononeka kwa kuona picha za machungu na mateso ya watu wake.'
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Al-Sudani amesema katika kikao hicho hicho cha Cairo: "Lau maneno ya taifa lenye haki halali yangesikilizwa na maazimio ya kimataifa kuheshimiwa, suala la Palestina lisingefikia hatua hii. Iraq inapinga suala la kuhamishwa kwa lazima Wapalestina kutoka Ukanda wa Ghaza na wakazi wake kuondoshwa makwao.Tunataka usitishwaji vita na kufunguliwa kwa vivuko ili misaada iwafikie haraka wakazi wa Ghaza na kisha kubadilishana mateka na wafungwa."
Tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa siku 16 zilizopita sawa na Oktoba 7, kushambuliwa maeneo ya makazi na umma kwa upande mmoja na kukatwa maji, umeme na uhaba mkubwa wa chakula na dawa kwa upande mwingine, kumewafanya wakazi wa Ukanda wa Ghaza kukabiliwa na hali ngumu sana na kupelekea taasisi za haki za binadamu kutangaza hali ya kibinadamu katika eneo hilo kuwa mbaya na ya kutisha. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa, UNICEF, Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Afya Duniani yamesema katika taarifa ya pamoja kwamba: "Tunatoa wito wa kusitishwa mapigano, pamoja na kufikishwa haraka misaada ya kibinadamu huko Ghaza, ili wanaoshughulikia misaada ya kibinadamu waweze kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji msaada, kuokoa maisha na kuwazuia kuendelea kupata mateso zaidi."
Kanali ya Televisheni ya Palestine Al-Yum imeripoti kuwa, mkurugenzi wa operesheni za UNRWA huko Ghaza amesema: "Hali ni mbaya sana na misaada ya kibinadamu ni midogo sana isiyoweza kukidhi mahitaji. Kuna uhaba mkubwa wa chakula na maji ya kunywa. Tunahitajia kudumishwa misaada ya kibinadamu ili kuzuia kuharibika zaidi hali ya ukanda huo. Siku ya Jumamosi, msafara wa kwanza ukiwa na malori 20 yaliyobeba misaada ya kibinadamu kutoka Hilali Nyekundu ya Misri, Shirika la Afya Duniani na Mpango wa Chakula Duniani uliingia Ukanda wa Ghaza baada ya kufunguliwa tena kwa muda kivuko cha Rafah. Hata hivyo, mafuta ambayo ni hitajio la dharura kwa wakazi wa eneo hilo si miongoni mwa bidhaa hizo, na kituo pekee cha kuzalisha umeme cha Ghaza kimefungwa kutokana na kukosekana mafuta, jenereta za hospitali nazo pia jazifanyi kazi, jambo ambalo linatishia maisha ya maelfu ya wagonjwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilitangaza Jumamosi kuwa lilisafirisha zaidi ya chupa 44,000 za maji ya kunywa katika Ukanda wa Ghaza kupitia kivuko cha Rafah, lakini kiasi hicho kwa siku moja kinatosha watu 22,000 pekee.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Kathryn Russell alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba hata kama misaada hiyo midogo ya kwanza huenda ikaokoa maisha ya baadhi ya watu, lakini misaada zaidi ya dharura inahitajika, sio tu maji, bali chakula, mafuta, dawa, na huduma nyingine muhimu. Amesema ikiwa misaada zaidi ya dharura ya kibinadamu haitafikishwa katika Ukanda wa Ghaza, basi wakazi wa ukanda huo watakabiliwa na tishio kubwa la kuenea magonjwa ya kuambukiza.
Baada ya sehemu kubwa ya miundombinu ya Ghaza, ikiwa ni pamoja na mifumo muhimu ya maji na maji taka, kuharibiwa katika mashambulizi ya zaidi ya wiki mbili ya utawala haramu wa Israel, uwezo wa uzalishaji maji katika eneo hilo umepungua hadi asilimia tano tu, wakati ambapo eneo la Ghaza lililo na takriban watu milioni mbili na laki tatu, linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji ambapo sasa kila mtu anaweza kupata chini ya lita tatu tu za maji kwa siku.
Kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa, karibu watu milioni moja wamehama makazi yao katika Ukanda wa Ghaza katika muda wa wiki mbili zilizopita, nusu yao wakiwa ni watoto, ambapo wengi wao wamekimbilia katika makazi yenye msongamano mkubwa wa watu na upatikanaji mdogo wa maji safi ya kunywa, mazingira ambayo ni hatari sana hasa kwa watoto wadogo.
Hayo yanajiri licha ya kwamba mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni yangali yanaendelea na kanali ya habari ya Al Jazeera ya Qatar ikinukuu ofisi ya habari ya serikali ya Ukanda wa Ghaza imesema kuwa, hospitali za eneo hilo zinapokea karibu mashahidi na majeruhi wapya 50 kila baada ya saa moja wengi wao wakiwe ni wanawake na watoto.
Harakati ya Kimataifa ya Kutetea Watoto imetangaza kuwa tangu kuanza Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba, utawala wa Kizayuni umeua zaidi ya watoto 1,661 huko Ghaza, ambao ni wastani wa watoto 120 kwa siku.
Mashambulio ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza katika kipindi cha siku 16 zilizopita yamesababisha kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina elfu 4, wengine elfu 13 wakijeruhiwa na milioni moja kuwa wakimbizi, idadi ambayo inaongezeka kila siku. Hivi sasa Ghaza inakabiliwa na hali mgumu sana ya kimaisha kuliko wakati mwingine wowote na kufikishwa huko haraka misaada ya kibinadamu kunaweza kupunguza kwa kiwango fulani hali hiyo. Pamoja na hayo, kuendelea mashambulizi, hasa ikiwa yataambatana na mashambulio ya nchi kavu, bila shaka kutavuruga zaidi hali mbaya ya eneo hilo.