Mitetemo ya Kimbunga cha Al Aqsa ndani ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103868-mitetemo_ya_kimbunga_cha_al_aqsa_ndani_ya_israel
Mgawanyiko na hitilafu zinazidi kuongezeka ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu tangu kuundwa serikali yenye misimamo mikali ya Netanyahu na kuenea hadi kwa raia wa kawaida; huku wafuasi wa makundi mawili ya kisekula na kidini wakikabiliana mara kadhaa hadi sasa na wakati mwingine wakijikita katika mapigano na kuibua ghasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2023 02:40 UTC
  • Mitetemo ya Kimbunga cha Al Aqsa ndani ya Israel

Mgawanyiko na hitilafu zinazidi kuongezeka ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu tangu kuundwa serikali yenye misimamo mikali ya Netanyahu na kuenea hadi kwa raia wa kawaida; huku wafuasi wa makundi mawili ya kisekula na kidini wakikabiliana mara kadhaa hadi sasa na wakati mwingine wakijikita katika mapigano na kuibua ghasia.

Mgawanyiko huu pia sasa umeenea hadi jeshini; ambapo uungaji mkono wa jeshi kwa wale wanaopinga kile kinachojulikana kama mswada wa marekebisho ya mahakama ndani ya utawala wa Kizayuni na wakati huo huo uungaji mkono wa Wizara ya Fedha na Usalama wa Ndani kwa Baraza la Mawaziri la Netanyahu kwa wanamgambo wenye silaha wanaopewa himaya na vyama vya mrengo wa kulia dhidi jeshi la utawala wa Kizayuni, umeibua mvutano na hitilafu kati ya serikali ya Benjamini Netanyahu na jeshi ambapo pande mbili hizo zimekuwa zikishambuliana kwa maneno mara kwa mara. 

Katika mazingira kama hayo, kutekelezwa operesheni ya kushtukiza ya "Kimbunga cha Al-Aqsa" ijapokuwa kumezisukuma ukingoni kwa siku kadhaa hitilafu na mivutano inayoshuhudiwa ndani ya utawala wa Kizayuni kutokana na mshtuko  uliousababishwa kwa utawala huo, lakini kushindwa serikali ya Netanyahu kukabiliana na operesheni hiyo kwa upande mmoja, na kupuuzwa suala la hatima ya mateka wa Israel  kinyume na taratibu za huko nyuma ni masuala mapya yaliyoibua hitilafu kubwa ndani ya utawala wa Kizayuni pamoja na kadhia nyingine zinazohusiana na oparesheni za nchi kavu. 

Kimbunga cha Al Aqsa 

Gazeti la Yediot Aharanot limeandika kuwa mawaziri watatu wa utawala wa Kizayuni wanataka kujiuzulu ili kumlazimisha Netanyahu akubali kuwajibika kufuatia kushindwa mbele ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, na asilimia 75 ya Wazayuni wanambebesha dhima Netanyahu ya kushindwa kuvilinda vitongoji vya walowezi kandokando ya Ukanda wa Ghaza. Wakati huo huo zaidi ya nusu ya wapiga kura wamekitaka chama tawala cha Likud pia kimuuzulu Netanyahu baada ya vita vya sasa huko Ghaza.  

Aidha katika maandamano ya maelfu ya watu Jumamosi iliyopita huko Tel Aviv, Wazayuni wengi ambao walimiminika mitaani dhidi ya serikali ya Netanyahu na utendaji wake mkabala wa oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa walipiga nara wakiiambia harakati ya Hamas kwamba wako tayari kuikabidhi Netanyahu mkabala wa kuachiwa huru watoto wao. 

Nadaf Eyal mchambuzi na mwandishi habari wa Kizayuni wa gazeti la Yediot Aharanot anasema: Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni bado yuko usingizini na baraza lake la mawaziri linaendeshwa bila ya mkakati wa wazi na unaoeleweka. 

Haim Bibas mwakilishi katika bunge la Israel (Knesset) ambaye pia ni mkuu wa serikali za mitaa wa utawala huo ametangaza kuwa baraza la mawaziri la Netanyahu bado halijaamka na limeshindwa kudhibiti hali ya mambo katika kipindi hiki cha dharura.  

Wakati huo huo kujiuzulu siku kadhaa zilizopita Galit Distel-Atbaryan Waziri wa Habari wa utawala wa Kizayuni na pia Waziri wa Afya wa utawala huo ni ishara ya hitilafu hizo tajwa zinazoendelea kutokota ndani ya serikali bandia ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hata hivyo hitilafu zote hizo haziishii katika mabadiliko hayo.  

Hitilafu hizo zimepelekea watu kama Yair Lapid mkuu wa sasa wa mrengo wa upinzani pia kukataa kujiunag na baraza la mawaziri la dharura. Baraza hilo liliundwa hivi karibuni likimshirikisha Benny Gantz na watu wengine kadhaa kama Gadi Eisenkot, ambapo hata hivyo watu kama Itamar Ben Gvir Waziri wa sasa wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni  waliwekwa kando.

Ben Gvir kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na chenye misimamo mikali cha Wazayuni cha (Uzayuni wa Kidini) ni miongoni mwa shakhsia wenye misimamo ya kufurutu ada walioko ndani ya muungano wa serikali ya Netanyahu, jambo ambalo pole pole limekuwa moja ya changamoto kuu za serikali hiyo.  

Itamar Ben Gvir

Uchunguzi wa maoni ulioendeshwa ndani ya Israel unaonyesha kuwa, chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kimepata upungufu mkubwa zaidi wa viti bungeni katika wiki za hivi karibuni, ambapo viti hivyo vimepungua kutoka viti 28 hadi viti 18  katika uchaguzi wa Oktoba 6, 2023 siku moja kabla ya kuanza vita. Bila shaka, tofauti hizo haziishii tu katika vyama na makundi ya kisiasa bali zimeenea pia miongoni mwa wakazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. 

Chunguzi za maoni zinaeleza kuwa, asilimia 80 ya wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wanaamini kuwa Netanyahu ndiye mkosa mkuu katika vita vinavyoendelea sasa; na  asilimia 70 ya wapiga kura wa chama cha Likud pia wanamnyooshea kidole cha lawama Netanyahu. 

Hii ni katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita maandamano makubwa yalifanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi ya utawala wa Kizayuni ambapo waandamanaji walikuwa wakipiga nara wakitaka kujiuzulu Netanyahu. Katika upande mwingine, kufuatia kuahirishwa mara kadhaa mpango wa mashambulizi ya nchi kavu ya utawala huo huko katika Ukanda wa Gaza, kumeibuka mgogoro wa "kutoaminiana" ndani ya baraza la mawaziri kati ya Waziri Mkuu na makamanda wa jeshi. Kutoelewana kuhusu namna ya kutekeleza mashambulizi ya nchi kavu, kumekigawa chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu, katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni la wale wanaomuunga mkono Netanyahu na maamuzi yake na kutaka kuingia Ghaza kupitia mashambulizi ya nchi kavu, huku wakiamini kuwa kuingia huko kusiwe kwa muda mrefu bali kuwe kwa muda mfupi tu yaani kuingia na kisha kuondoka katika ukanda huo. 

Maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu dhidi ya Benjamin Netanyahu 

Kundi la pili ni la wale wanaosema kuwa jeshi linapaswa kuingia kikamilifu Ghaza; kisha  liliangamize Hamas na hatimaye kuikalia  kwa mabavu kikamilifu Ghaza. Na  kundi la tatu  linaamini kuwa, vita hivyo vinapasa kumalizika haraka iwezekanavyo na hatima ya mateka ijulikane kupitia mazungumzo. Pamoja na hayo, Wazayuni wanafahamu vyema kuhusu ugumu wa mashambulizi ya nchi kavu dhidi ya Ukanda wa Ghaza na uwezekano wa kupata kipigo kingine kikali kutoka kwa makundi ya mapambano. 

Mwaka 2014 pia jeshi la Israel liliingia Ghaza hata hivyo hatimaye lililazimika kuondoka eneo hilo baada ya kupoteza vikosi vyake. Mwaka 2005 pia serikali ya wakati huo ya Israel chini ya Waziri Mkuu Ariel Sharon na ambayo kipindi hicho ilikuwa inaikalia Ghaza kwa mabavu ililazimika kuondoka katika eneo hilo kwa madhila.  Kwa mtazamo huo, kinachofanywa sasa na vikosi vya wanamuqawama ni kuhesabu muda tu wa jeshi la Kizayuni kuingia Ghaza ili viweze kulipiza kisasi kwa mashambulio na hujuma kubwa dhidi ya raia wa Palestina, hujuma ya jinai ambayo hadi sasa imesababisha kuuliwa na kujeruhiwa karibu watu elfu 20 na kusababisha wakazi wengine wa Ghaza zaidi ya milioni moja kuwa wakimbizi. 

Wanamuqawama wa Palestina