Amnesty yataka kusitishwa uanachama wa Saudia katika Baraza la Haki Binadamu
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kwa mara nyingine tena limetoa wito wa kusimamishwa uanachama wa Saudi Arabia katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Amnesty International imetaka kusimamishwa uanachama wa Saudia katika baraza hilo na kutangaza kuwa, tangu ilipojiunga na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Saudi Arabia imewanyonga watu 350 na inaendelea kuwakandamiza na kuwatesa wapinzani na watetezi wa haki za binadamu.
Taarifa hiyo imeongeza kwa kuhoji kuwa: Ni kwa haki ipi Saudia ikapewa uongozi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa? Amnesty International imesema Saudi Arabia inashambulia na kubomoa hospitali nchini Yemen bila ya kufuatiwa au kuadhibiwa.
Kwa msingi huo Amnesty International imesema Saudia inapaswa kupokonywa uanachama wake katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa sababu inatumia vibaya nafasi hiyo kwa ajili ya kuficha ya kufunika jinai na ukatili wake katika maeneo mblimbali.
Maelfu ya raia wasio na hatia nchini Yemen wameuawa kufuatia mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya maeneo ya umma kama misikiti, hospitali na shule.