Wapalestina sasa wazika mashahidi wao katika makaburi ya umati
Habari kutoka Ukanda wa Gaza zinaarifu kuwa, kutokana na kushtadi mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa Israel na kuongezeka kwa kiwango cha kutisha idadi ya wananchi wa Palestina wanaouawa shahidi katika eneo hilo, Wapalestina hivi sasa wanalazimika kuwazidi mashahidi wao katika makaburi ya halaiki.
Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, idadi kubwa ya wahanga wa hujuma za kinyama za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza imepelekea mashahidi kuzikwa bila kufanyiwa taratibu za kawaida za Kiislamu, kama kuoshwa, kukafiniwa, na kuswaliwa; na sasa wanazikwa kwa wingi katika makaburi ya umati.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kutokana na mashambulio hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo inakaribia watu 10,000.
Oktoba 7, 2023, vikosi vya Muqawama wa Palestina vilianzisha operesheni ya kushtukiza iliyopewa jina la Kimbunga cha Aal-Aqsa kutokea Gaza (kusini mwa Palestina) dhidi ya ngome za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Katika hatua ya kulipiza kisasi na kufidia kipigo kikali na pigo kubwa ulilopata, utawala wa Kizayuni umechukua hatua ya kufunga vivuko vyote vya Gaza na hivi sasa unaendeleza mashambulio ya mtawalia dhidi ya maeneo ya makazi ya watu na vituo vya tiba vya Ukanda huo.

Watoto wadogo, wanawake na vikongwe ndio wahanga wakuu wa jinai hizo za kutisha za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza, kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi.
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, Martin Griffiths anasema eneo la Gaza limegeuka kuwa makaburi kwa watoto kwani maelfu wameuawa kufuatia mashambulizi yanayofanywa na utawala haramu wa Israel, huku zaidi ya watoto milioni moja wakikabilwa na uhaba wa mahitaij muhimu na maisha yao ya baadaye yakiwa mashakani.