Jul 07, 2016 04:21 UTC
  • Wakuu wa Saudia wanafanya biashara ya mihadarati wakati wa Hija

Maafisa wa ngazi za juu katika ufalme wa Saudi Arabia wamekuwa wakiingiza dawa za kulevya nchini humo kwa kutumia mabasi yanayowabeba mahujaji, imefichuliwa.

Afisa wa kijeshi mwenye cheo cha meja ambaye aliwahi kufanya kazi katika Idara ya Kupambana na Mihadarati ya Wizara ya Mambo ya Ndani amekamatwa baada ya kufichua kuhusu mtandao huo wenye nguvu wa uingizaji dawa za kulevya Saudia.

Meja Turki bin Hamza al-Rashidi amesema kuwa, mtandao wenye nguvu wa watu walio karibu na watawala wa kifalme Saudia wametengeneza mabilioni ya dola kwa kuingiza dawa za kulevya Saudia kwa njia mbali mbali.

Katika jumbe kadhaa alizotuma katika mtandao wa Youtube, Meja Rashidi anasema kuwa moja ya mbinu zilizokuwa zikitumiwa ni ile ya "mchezo wa mabasi pacha." Mbinu hiyo ilikuwa ikihusisha basi lililojaa Mahujaji wa kawaida waliokuwa wakielekea Makka kwa ajili ya Ibada ya Hija. Mabasi hayo yalikuwa yakipita eneo la forodha mpakani na kupewa nyaraka za kuidhinisha kuwa wasafiri na mizigo ni ya mahujaji. Nyaraka hizo hizo zilikuwa zikitumiwa baadaye kuruhusu basi lililojaa mihadarati kuingia katika ufalme huo.

Meja Rashidi anasema alipata ushahidi uliowahusisha maafisa wa ngazi za juu katika Ufalme wa Saudia katika kashfa hiyo ya kutumia mabasi ya Mahujaji kuingiza mihadarati katika ufalme huo. Afisa huyo hivi sasa amekamatwa na ametuma ujumbe akisema anahofia maisha yake.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Mwanamfalme Abdel Mohsen bin Walid bin Abdulaziz kutoka ukoo wa kifalme wa Aal Saud alitiwa mbaroni katika Uwanja wa Ndege wa Beirut Lebanon akiwa na shehena kubwa ya mihadarati aina ya captagon na cocaine katika ndege yake binafsi.

Tags