Hukumu ya kifungo cha miaka 10 jela dhidi ya Imran Khan
Mahakama ya Nyaraka za Siri ya Pakistan imemhukumu Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Imran Khan na msaidizi wake wa karibu, waziri wa zamani wa mashauuri ya Kigeni Shah Mahmood Qureshi, kifungo cha miaka 10 jela katika kesi inayohusiana na uvujishaji wa siri za serikali.
Mahakama maalumu iliyoundwa ndani ya gereza la Rawalpindi, siku ya Jumanne ilitangaza hukumu hiyo katika kesi iliyopewa jina la 'cypher', inayohusiana na kebo ya kidiplomasia ambayo Khan anadai inathibitisha madai yake kwamba, kuondolewa kwake madarakani mwaka 2022 kulitokana na njama iliyohusisha serikali ya Marekani.
Mahakama iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Siri Rasmi ilimpata Khan na hatia ya kutumia vibaya kebo hiyo ya siri iliyotumwa na balozi wa zamani wa Pakistan nchini Marekani.
Duru za Pakistan ziliripoti kuhusiana na habari hiyo kwamba, baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi wa mahakama wa faili la kesi ya ufichuzi wa nyaraka za siri, hatimaye chombo hicho kimewapata na hatia maafisa wawili wakuu wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf ambao pia ni maafisa wa serikali ya zamani ya Pakistani na hivyo kuwahukumu kifungo cha miaka 10 jela.
Seneta Ali Zafar, afisa mkuu wa chama cha Tehreek-e-Insaf na mkuu wa timu ya wanasheria ya Imran Khan, aliuchukulia uamuzi wa mahakama hiyo kuwa wa upande mmoja na akatangaza kwamba atapinga uamuzi huo katika Mahakama ya Juu haraka iwezekanavyo.
Katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi wa mwezi Aprili mwaka huu, baadhi ya duru za kisiasa nchini Pakistan zinaweza kuutathmini uamuzi huo kama wenye matashi ya kisiasa, kwa sababu utendaji huo unaonekana uko tofauti na ilivyokuwa katika kesi zilizokuwa zikimkabili Waziri Mkuu wa zamani Muhammad Nawaz Sharif.
Abbas Fayaz, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Mfumo wa mahakama nchini Pakistan unachukuliwa kuwa huru. Hata hivyo, chama cha Tehreek-e-Insaf kimetangaza kuwa, kinapinga hukumu iliyotolewa dhidi ya maafisa wake wakuu. Pamoja na hayo, pigo la kuzuiwa Imran Khan kushiriki katika uchaguzi ujao ni chungu zaidi kwa chama cha Tehreek-e-Insaf.
Kabla ya hapo viongozi wa Pakistan Tehreek-e-Insaf walipinga vikali mchakato wa kesi ya Imran Khan na kusisitiza kwamba, hakuna nyenzo zozote zilizotolewa kwa Waziri Mkuu na Waziri wa zamani wa Mashaauri ya Kigeni wa nchi hiyo kwa ajili ya kuwa na wakili binafsi na kujitetea mahakamani.
Tehreek-e-Insaf, ambacho kilikuwa chama cha kijimbo huko Khyber Pakhtunkhwa, ghafla na haraka kiligeuka na kuwa chama cha kitaifa kwa kuungwa mkono na jeshi na mahakama, jambo ambalo lilipelekea kuondolewa madarakani Muhammad Nawaz Sharif kwa kuvuliwa uwaziri mkuu. Hata hivyo, upinzani wa Imran Khan dhidi ya Marekani, hasa katika vita vya Ukraine, kulipelekea naye aondolewe madarakani kwa kura ya Bunge, na sasa kwa kufungwa kwake, inawezekana kusema kwamba, Tehreek-e-Insaf kinaweza kufutwa kabisa katika ulingo wa siasa za Pakistan.
Hii ni kutokana na kuwa, katika jamii ya kisiasa ya Pakistan ilikuwa ikionekana kwamba kuwepo kwa Tehreek-e-Insaf katika uwanja wa siasa za nchi hiyo kunamaanisha kuvunjwa anga ya kambi mbili za vyama vya Muslim League-Nawaz na Pakistan Peoples Muslim League. Kwa hivyo, kwa kufungwa Imran Khan na kudhoofika sana nafasi ya Tehreek-e-Insaf katika uchaguzi ujao, kunaweza kuelezwa kwamba, uwanja huo umeandaliwa kwa ajili ya uchaguzi kuwa katika kambi mbili na kushadidi tena ushindani kati ya Muslim League-Nawaz na Pakistan Peoples Muslim League. Pamoja na hayo inaonekana kwamba, uwanja na mazingira yameandaliwa kwa ajili ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi ujao chama cha Muslim League cha Nawaz Sharif ili kwa kushika tena Muhammad Nawaz Sharif cheo cha Waziri Mkuu afanye hima ya kutatua changamoto za kieneo na kimataifa zinazoikabili Pakistan.
Ni kwa sababu hiyo, ndio maana chama cha Tehreek-e-Insaf daima kimeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu utendaji wa kibaguzi dhidi ya wanachama wa chama hiki na kuwazuia kushiriki katika uchaguzi ujao nchini Pakistan.
Kwa kuzingatia kuwa, Imran Khan yuko gerezani akihusishwa na kesi kadha wa kadha za ufisadi wa kifedha, kisiasa na kiusalama, uwezekano kwamba atahukumiwa na mahakama katika kesi hizo ni jambo ambalo haliko mbali. Kwa muktadha huo, inaonekana kwamba, timu ya wanasheria ya Imran Khan itapigana kuufa na kupona na kufanya kila iwezalo kupinga kifungo hicho cha miaka kumi jela dhidi ya mteja wao.
Alaa kulli haal, inaonekana kwamba vyama viwili vya Muslim League Nawaz na Pakistan Peoples Muslim League vimefurahia na kupokea kwa mikono miwili hukumu ya kifungo cha miaka kumi jela dhidi ya Imran Khan na kudhoofika chama chake katika uchaguzi ujao; kwani hatua hiyo itahifadhi na kubakisha mazingira ya ushindani baina ya kambi mbili hizo.