Mateka wa Kizayuni; mgogoro usio na kikomo kwa Benjamin Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108014-mateka_wa_kizayuni_mgogoro_usio_na_kikomo_kwa_benjamin_netanyahu
Kuendelea maandamano katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya kutaka kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni, kumegeuka na kuwa mgogoro na jinamizi linalomkaba koo Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu pamoja na baraza lake la mawaziri.
(last modified 2024-02-05T02:57:08+00:00 )
Feb 05, 2024 02:57 UTC
  • Mateka wa Kizayuni; mgogoro usio na kikomo kwa Benjamin Netanyahu

Kuendelea maandamano katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya kutaka kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni, kumegeuka na kuwa mgogoro na jinamizi linalomkaba koo Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu pamoja na baraza lake la mawaziri.

Katika muendelezo wa maandamano hayo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, siku ya Jumamosi tarehe 3 Februari baadhi ya walowezi wa Kizayuni walifanya maandamano katikati mwa Tel Aviv kwa lengo la kushinikiza kuharakishwa makubaliano ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya kushindwa juhudi za utawala wa Kizayuni za kuwakomboa mateka hao kwa kutumia mabavu na kuyashambulia maeneo tofauti ya Gaza. Wiki iliyopita, sambamba na kikao cha baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni cha kujadili kuhusiana na makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, familia za mateka wa Israel zilifanya maandamano mjini Tel Aviv kwa ajili ya kutaka utekelezwaji wa makubaliano ya kubadilishana mateka na kutoa mwito wa kuvunjwa baraza la mawaziri la Netanyahu na kufanyika kwa uchaguzi wa mapema wa Bunge.

Wawakilishi wa utawala wa Kizayuni, Marekani, Misri na Qatar hapo awali walifikia makubaliano mjini Paris, Ufaransa kuhusu fremu ya kusimamisha vita na kuwaachia huru mateka wengine wa jeshi la utawala huo ghasibu wa Israel na Hamas.

Viongozi wa Hama na Jihadul Islami wakionyesha mshikamano wao

 

Harakati mbili za Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihadul Islami zimesema kuwa, mapendekezo yoyote ambayo hayatopelekea kusimamishwa kikamilifu uvamizi wa Israel huko Gaza, hayakubaliki kwa namna yoyote ile.

Hamas na Jihadul Islami zinasisitiza kuwa, mazungumzo yoyote ambayo hayatopelekea kumalizwa vita na kuondoka wanajeshi vamizi wa Israel nje ya Ukanda Gaza pamoja na kuhitimishwa mzingiro na kujengwa upya ukanda huo hayawezi kukubaliwa na harakati hizo, na hakuna mabadilishano yoyote ya mateka maadamu masharti hayo hayajatimia.

Maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Neytanyahu yamekuwa yakiendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ambazo zimepewa jina bandia la Israel tangu Oktoba 7 mwaka jana (2023) wakati kulipotekelezwa na muqawama operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa.

Waandamanaji hao wanasisitiza kuwa, baraza la mawaziri la Netanyahu limeshindwa kuwarejesha mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Hamas. Mamlaka za utawala wa Kizayuni huficha takwimu kamili za wafungwa wao wa kijeshi, lakini idadi yao inakadiriwa kuwa ni mamia.

Baadhi ya mateka wa Israel waliokuwa wakishikiliwa na Hamas wakiachiliwa huru katika moja ya mapatano ya mabadilishano ya mateka baina ya Hamas na Israel

 

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na Wazayuni wenye misimamo ya kuchupa mipaka ambao wanaunda serikali ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya utawala ghasibu wa Israel daima wamekuwa wakiahidi ushindi wa haraka dhidi ya Hamas na kuwarejesha mateka wa Kizayuni tangu mwanzoni mwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa. Lakini kwa kupita muda na kuendelea kwa operesheni za makundi ya wapiganaji wa Palestina, matokeo ya ahadi yamekuwa ni hewa tupu kutokana na ahadi hizo kutotekelezwa. Hali hiyo imewafanya baadhi ya viongozi wa utawala huo kujitokeza na kukiri hadharani juu ya kushindwa utawala huo na muqawama wa Palestina.

Yossi Cohen, mkuu wa zamani wa Shirika la Kijajsusi la Israel MOSSAD amesema kuwa, ili kuwarejesha mateka Israel kutoka Gaza, utawala wa Kizayuni unapaswa kulipa gharama kubwa mno.

Maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yanaendelea katika hali ambayo, wakuu wa utawala wa Kizayuni walilazimika kukubali masharti ya Hamas ya usitishaji vita jambo ambalo liliweka wazi udhaifu wa Israel mbele ya wanamuqawama shupavu wa Palestina.

Ukweli wa mambo ni kuwa, makundi ya muqawama wa Palestina yalifanikiwa ipasavyo kubadilisha mlingano baada ya operesheni ya tarehe 7 Oktoba, na kuendelea kusimama kwao kidete kumepelekea udhaifu wa Israel uzidi kudhihirika zaidi siku baada ya siku.

Kushadidi mgogoro wa kiuchumi kutokana na kuendelea vita vya Tel Aviv, nafasi legevu na tepetevu ya baraza la mawaziri la muungano huko Israel, kuendelea maandamano katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kufichuliwa ukweli wa kudhurika kiusalama utawala wa Kizayuni mkabala wa udhibiti wa taarifa za kiintelijensia na kioperesheni wa makundi ya muqawama wa Palestina ni sehemu ya matunda na mafanikio ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa.

 

 

Utawala wa Kizayuni uko katika hali mbaya licha ya uungaji mkono wa kifedha, kisiasa na pia wa matangazo wa makampuni ya utangazaji ya habari nchini Marekani na Ulaya. Kuendelea kwa maandamano hayo bila shaka kutakuwa ni fursa kwa vyama vya upinzani katika Bunge la Israel “Knesset” kuendeleza lengo lao la kuwafungulia mashtaka na kuliondoa madarakani baraza la sasa la mawaziri linaloongozwa na Netanyahu ambaye yeye pia anakabiliwa na mafaiili kadhaa ya kesi za ufisadi.

Lililo dhahir shahir ni kwamba, baraza la mawaziri la Netanyahu na mamlaka za utawala wa Kizayuni zinakabiliwa na mgogoro na maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kiasi kwamba, kuendelea hali hiyo kumewafanya washirika wao wa Marekani na Magharibi, kutilia shaka uwezo wa Tel Aviv wa kuwajibika kwa ajili ya utekelezaji wa usitishaji vita na kutekeleza ahadi zake.

Utawala wa Kizayuni una historia ndefu ya kuvunja ahadi na kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa na utekelezwaji wake katika nyakati tofauti katika miaka ya hivi karibuni, na hali mbaya ya ardhi inayokaliwa kwa mabavu itakuwa ni kisingizio kwa Netanyahu na baraza lake la mawaziri lenye misimamo ya kupindukia cha kukwepa kutimiza ahadi na wajibu wao wa kimataifa.