Wapalestina wengine 14 wauawa shahidi; US, UK zaendeleza mashambulizi Yemen
Wapalestina wengine 14 wauawa shahidi katika kambi ya wakimbizi ya al Nasirat katikati mwa Ukanda wa Ghaza baada ya wanajeshi makatili wa Kizayuni kufanya mashambulizi kwenye maeneo ya raia. Jinai hiyo imefanyika huku Marekani na Uingereza nazo zikiendelea kuishambulia Yemen ili kuunga mkono jinai za Israel huko Ghaza.
Shirika la habari la IRNA limenukuu taarifa ya karibuni kabisa ya Wizara ya Afya ya Ghaza ikisema kuwa, utawala wa Kizayuni umefanya jinai nyingine kubwa kwa kushambulia kikatili maeneo ya raia na kusababisha wananchi 103 wa Palestina kuuawa shahidi na wengine 145 kujeruhiwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo hivi sasa siku 131 zimepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza hapo tarehe 7 Oktoba 2023 na mpaka sasa Wapalestina 28,576 wamethibitishwa kuuawa shahidi na 68,291 wameshajeruhiwa kwenye jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya hivi karibuni.
Huku hayo yakiripotiwa, Marekani na Uingereza ambazo ni waungaji mkono wakuu wa kila upande wa jinai za Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia huko Palestina hasa Ghaza, wameendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo tofauti ya Yemen kutokana na wananchi Waislamu wa Yemen kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina.
Televisheni ya Al Mayadeen imeripoti kuwa, madola vamizi na ya kiistikbari ya Marekani na Uingereza yamefanya mashambulizi mapya katika maeneo ya al Haj na Bait al Faqih kwenye mkoa wa al Hudaidah, magharibi mwa Yemen.
Wamefanya mashambulio pia kwa kutumia ndege za kivita kwenye maeneo ya al Jabanah na Ra's Isa kwenye mkoa huo wa al Hudaidah ili kuwalazimisha wananchi wa Yemen waache kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina hasa wa Ghaza.