Ripoti: Nchi za Kiarabu hazitaki Marekani itumie ardhi zao kuishambulia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108480-ripoti_nchi_za_kiarabu_hazitaki_marekani_itumie_ardhi_zao_kuishambulia_iran
Nchi kadhaa za Kiarabu zinaripotiwa kukataa maombi ya Marekani na washirika wake kufanya mashambulizi kutoka katika ardhi zao dhidi ya Iran na makundi ya muqawama katika eneo la Asia Magharibi wakati huu wa mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Feb 17, 2024 04:12 UTC
  • Ripoti: Nchi za Kiarabu hazitaki Marekani itumie ardhi zao kuishambulia Iran

Nchi kadhaa za Kiarabu zinaripotiwa kukataa maombi ya Marekani na washirika wake kufanya mashambulizi kutoka katika ardhi zao dhidi ya Iran na makundi ya muqawama katika eneo la Asia Magharibi wakati huu wa mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Jarida la Kimarekani la Politico lilimnukuu afisa mmoja wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa akisema kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu, zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, zimeweka vikwazo kwa Marekani kuhusu kutumia kambi zake za kijeshi ndani ya ardhi zao kwa kufanya mashambulizi dhidi ya Iran na makundi ya muqawama au mapambano ya Kiislamu.

Jarida hilo limeripoti kuwa, vikwazo hivyo pia vinajumuisha oparesheni dhidi ya makundi ya muqawama Iraq, Syria na Bahari ya Shamu.

Jarida hilo la mtandaoni la Marekani halikuweka wazi majina na idadi kamili ya nchi za Kiarabu zinazohusika katika kuzuia Marekani kutumia ardhi zao kwa ajili ya kuishambulia Iran na makundi ya mapambano ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.

Kulingana na Politico, afisa huyo amesema kuwa sababu maalumu ya UAE kuchukua hatua kama hiyo ni kwamba viongozi wa nchi hiyo hawataki kuonekana kama wanapingana na Iran na hawataki kuonekana karibu sana na Magharibi na Israeli, kwani hilo litapelekea wachukiwe na umma.

Hivi karibuni vikosi vamizi vya Marekani na washirika kadhaa wa Washington vimezidisha mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi kwa ajili ya kuunga mkono utawala wa Israel ambao tangu mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Kituo cha jeshi vamizi la Marekani cha Tower 22 kililengwa na wanamuqawama

Zaidi ya Wapalestina 28,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa na wengine zaidi ya 68,000 kujeruhiwa tangu utawala wa Israel uanzishe hujuma yake iliyoungwa mkono na Marekani huko Gaza Oktoba 7, 2023.

Yemen imetangaza vita vya wazi dhidi ya maslahi ya Marekani na Uingereza tangu nchi hizo mbili zianzishe kampeni ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu kuunga mkono Israel.

Iran kwa nyakati tofauti imekuwa ikisisitiza kuwa haina makundi yanayopigana kwa niaba yake katika eneo la Magharibi mwa Asia. Hii ni baada ya Marekani kudai kuwa "washirika" wa Iran wanahusika katika mashambulizi dhidi ya vikosi vyake Asia Magharibi. Iran imesisitiza kuwa makundi ya muqawama yanajitegemea na hayachukui amri yoyote kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu.