Sayyid Nasrullah: Israel 'italipa kwa damu' mauaji ya raia wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108488-sayyid_nasrullah_israel_'italipa_kwa_damu'_mauaji_ya_raia_wa_lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema utawala wa Israel "utalipa kwa damu" gharama ya mauaji ya hivi karibuni ya raia kusini mwa nchi hiyo, akisisitiza kwamba mauaji hayo hayawezi kuifanya harakati hiyo kuacha kuwaunga mkono na kuwatetea Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
(last modified 2024-02-17T04:40:00+00:00 )
Feb 17, 2024 04:40 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema utawala wa Israel "utalipa kwa damu" gharama ya mauaji ya hivi karibuni ya raia kusini mwa nchi hiyo, akisisitiza kwamba mauaji hayo hayawezi kuifanya harakati hiyo kuacha kuwaunga mkono na kuwatetea Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Sayyid Hassan Nasrullah alisema hayo katika hotuba yake ya televisheni iliyotangazwa moja kwa moja kutoka mji mkuu wa Lebanon,, Beirut siku ya Ijumaa kwa mnasaba wa Siku ya Viongozi wa Hizbullah Waliouawa Shahidi, ambayo huadhimishwa kila mwaka Februari 16.

Hotuba hiyo imekuja siku mbili baada ya utawala wa Israel kulenga jengo moja katika mji wa Nabatiyeh kusini mwa Lebanon, na kuua watu saba wa familia moja, akiwemo mtoto.

Katika shambulio jingine la utawala huo haramu, mwanamke mmoja na watoto wake wawili pia waliuawa katika kijiji cha as-Sawana kusini mwa Lebanon.

Nasrullah amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Nabatiyeh na as-Sawana akiyataja kuwa ni "mauaji ya kimakusudi," na akasema Tel Aviv lazima ijue kwamba "ilikwenda mbali sana" kwa kuwalenga raia.

Akisisitiza kuwa lengo la utawala wa Israel la kuua raia ni kushinikiza kukomeshwa muqawama au mapambano, Nasrullah amesema: "Tuko katika kitovu cha vita vya kweli kwenye mstari ambao una urefu wa zaidi ya kilomita 100, na kuuawa shahidi wapiganaji wetu ni sehemu ya vita.

Kombora la Hizbullah likiwa linavurumishwa kuelekea vitongoji vya Wazayuni

Kiongozi huyo wa Hizbullah amesema kulengwa hivi karibuni kwa kitongoji haramu cha walowezi wa Kizayuni cha Kiryat Shmona kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa makombora kadhaa ya Katyusha ni "jibu la awali" kwa umwagaji damu wa Jumatano, na kuongeza kuwa wanamapambano wa Lebanon wana uwezo mkubwa na sahihi wa makombora ambayo yanaweza kulenga Kiryat Shmona kaskazini hadi Eilat kusini.

Sayyid Hassan Nasrullah aidha amesema: "Licha ya kila kitu ambacho adui na Wazayuni wanafanya katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza, Wamarekani na Waisraeli lazima waelewe kwamba, huko Palestina wanakabiliwa na watu ambao hawatarudi nyuma.".

Nasrullah pia amewashukuru wanajeshi wa Yemen kwa kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya meli za Marekani na Uingereza katika Bahari ya Sham kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina na kusisitiza kuwa vita kuu ni Gaza.

Mkuu huyo wa Hizbullah ameilaumu vikali Washington kwa uungaji mkono wake usiosita kwa Israel katika vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza na kusema maafisa wa Marekani "wanawajibika hasa kwa kila tone la damu inayomwagika katika eneo hilo."