Mohammad Nazal: Yahya Sinwar ni mzima na anaongoza mapambano Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108588-mohammad_nazal_yahya_sinwar_ni_mzima_na_anaongoza_mapambano_ghaza
Mjumbe mmoja mwandamizi wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, Yahya Sinwar ni mzima na anaendelea na shughuli zake za kuiongoza harakati hiyo ndani ya Ukanda wa Ghaza na kwamba atabakia kwenye wadhifa huo na hakuna hitilafu zozote kwenye safu ya viongozi wa HAMAS.
(last modified 2024-02-20T01:03:47+00:00 )
Feb 20, 2024 01:03 UTC
  • Yahya Sinwar
    Yahya Sinwar

Mjumbe mmoja mwandamizi wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, Yahya Sinwar ni mzima na anaendelea na shughuli zake za kuiongoza harakati hiyo ndani ya Ukanda wa Ghaza na kwamba atabakia kwenye wadhifa huo na hakuna hitilafu zozote kwenye safu ya viongozi wa HAMAS.

Mohammad Nazal amesema hayo kukanusha madai ya uongo ya waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni, Yoav Gallant aliyedai kuwa eti uongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hivi sasa unatafuta kiongozi mwingine wa kuchukua nafasi ya Yahya Sinwar.

Mohammad Nazal ameiambia televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kwamba, madai ya utawala wa Kizayuni kuhusu uwezo wa muqawama wa Palestina hayana ukweli wowote kwani sehemu kubwa ya wanamapambano wa Palestina wanaendelea na mapambano ndani ya Ukanda wa Ghaza.

 

Amesisitiza kuwa, HAMAS inataka kufikiwa makubaliano ya kubadilishana mateka lakini waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu anajaribu kupoteza muda na kuishinikiza Harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Ameongeza kuwa, Marekani inao uwezo wa kumlazimisha Netanyahu na utawala wa Kizayuni kukubali kuundwa nchi huru ya Palestina lakini haitaki na tusitarajie kuwa kuna siku itafanya jambo kama hilo.

Katika hatua ambayo viongozi wa Palestina wameiita kuwa ni vita vya kisaikolojia, waziri wa vita wa utawala katili wa Israel, Yoav Gallant alikuwa amedai kwamba kuna mpasuko katika safu za viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hasa kati ya wale walioko ndani ya Ghaza na wale walioko nje ya Palestina, lakini madai hayo yamekanushwa vikali na viongozi wa HAMAS ambao wamesisitiza kuwa, kiongozi wa harakati hiyo ndani ya Ghaza, Yahya Sinwar ni mzima na ataendelea kuiongoza harakati hiyo kwenye vita vinavyoendelea ndani ya ukanda huo hadi ushindi.