Hamas yalaani muswada wa Knesset unaopinga kuasisiwa nchi huru ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108674-hamas_yalaani_muswada_wa_knesset_unaopinga_kuasisiwa_nchi_huru_ya_palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana ililaani muswada wa bunge la Israel (Knesset) wa kutoitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
(last modified 2024-02-22T03:52:11+00:00 )
Feb 22, 2024 03:52 UTC
  • Hamas yalaani muswada wa Knesset unaopinga kuasisiwa nchi huru ya Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana ililaani muswada wa bunge la Israel (Knesset) wa kutoitambua rasmi nchi huru ya Palestina.

Shirika la habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, Hamas imetangaza katika taarifa yake kuwa muswada uliowasilishwa na bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuitoitambua rasmi nchi huru ya Palestina ni muendelezo wa siasa za utawala wa Kinazi na kuwanyima wananchi wa Palestina haki ya kuwa uhuru na kujitawala, na pia ni kuipuuza jamii ya kimataifa na maazimio ya kimataifa.

Hamas imesisitiza pia kwamba: Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zitakabiliwa na mtihani halisi wa kupinga maazimio na maamuzi ya utawala huo. Utawala wa Kizayuni unatekeleza haya yote lengo likiwa ni kufuta sura halisi ya kadhia ya Palestina kupitia mauaji ya kimbari yanayoungwa mkono na serikali ya Marekani. 

Harakati ya Hamas imeongeza kusema kuwa: Inataraji kuwa jamii ya kimataifa itaunga mkono na kutetea haki ya watu wa Palestina ya kujiainishia mustakbali wao, itatambua rasmi nchi huru ya Palestina na kuunga mkono mamlaka kamili ya kujitawala Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds Tukufu.  

Jana Jumatano vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilitangaza kuwa bunge la utawala huo ghasibu (Knesset) limeafiki pendekezo la baraza la mawaziri la kupinga kutambuliwa rasmi kwa upande mmoja nchi huru ya Palestina. 

Kuidhinishwa muswada huo wa baraza la mawaziri la Netanyahu ndani ya Knesset kumepingwa na Yair Lapid, kiongozi wa mrengo wa upinzani na waziri mkuu wa zamani wa Israel. 

Yair Lapid 

Yair Lapid amemkosoa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, akisema kuwa ameibua tishio jipya kwa Israel.