Hizbullah ya Lebanon yazitwanga kwa makombora kambi nne za Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108688-hizbullah_ya_lebanon_yazitwanga_kwa_makombora_kambi_nne_za_wazayuni
Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umetangaza kuwa, wanamapambano wa Hizbullah wameshambulia kwa makombora kundi la wanajeshi vamizi wa Israel katika kambi kadhaa tofauti za kijeshi za utawala wa Kizayuni.
(last modified 2024-02-22T08:02:51+00:00 )
Feb 22, 2024 08:02 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon yazitwanga kwa makombora kambi nne za Wazayuni

Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umetangaza kuwa, wanamapambano wa Hizbullah wameshambulia kwa makombora kundi la wanajeshi vamizi wa Israel katika kambi kadhaa tofauti za kijeshi za utawala wa Kizayuni.

Hizbullah ya Lebanon imesema katika taarifa yake kwamba imezipiga kwa makombora kambi nne za kijeshi za Israel ikiwemo ile ya Zabdin wakati wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walipokuwa wamekusanyika hapo.

Taarifa ya Hizbullah ya Lebanon imeongeza kuwa, mashambulizi yake hayo ya kulipiza kisasi na ya kuwaunga mkono wananchi wa Ghazza, yamewasababishia hasara za roho na mali wanajeshi makatili wa Israel. 

Siku chache tu zilizopita, mkuu wa baraza la kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Margaliot ambaye hivi karibuni aliliomba jeshi la Israel liharibu miji ya mpakani ya Lebanon, alikiri kwamba, mashambulio ya harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ni makali mno kiasi kwamba hawawezi tena kuingia na kutoka kwa urahisi katika mji huo na kitu pekee wanachoweza kufanya ni kujificha.

Mashambulizi ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya Wazayuni ni ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars; Eitan Davidi amesema hayo kufuatia mashambulizi makubwa ya maroketi ya Hizbullah dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye mipaka ya Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, na kuongeza kwa kusema: "Hali hapa si nzuri hata kidogo na hatuwezi kuingia na kutoka wakati wowote tunapotaka."

Kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni vilevile imemnukuu mkuu huyo wa kitongoji cha walowezi wa Kizayuni wa Margaliot akisema: "Hatuwezi kuendesha gari wakati wowote tunapotaka. Tunapokuwepo Margaliot huwa tunajificha kwenye mahandaki."

Hadi hivi sasa makumi ya maelfu ya walowezi wa Kizayuni wamekimbia kutoka kwenye vitongoji vya Kizayuni karibu na mpaka wa Lebanon kwa kuhofia vipigo kutoka kwa Hizbullah.