OIC yailaani Israel kwa mauaji ya kimbari ya raia Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108824-oic_yailaani_israel_kwa_mauaji_ya_kimbari_ya_raia_wapalestina_gaza
Mawaziri wa habari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wamelaani "ukandamizaji wa kimfumo na mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina" huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Feb 26, 2024 03:15 UTC
  • OIC yailaani Israel kwa mauaji ya kimbari ya raia Wapalestina Gaza

Mawaziri wa habari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wamelaani "ukandamizaji wa kimfumo na mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina" huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao kisicho cha kawaida kilichofanyika katika mji wa bandari wa Uturuki wa Istanbul, mawaziri wa habari wa nchi wanachama wameutaka utawala ghasibu wa Israel "kusitisha mapigano bila masharti" ili kuzuia hasara zaidi ya maisha ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Pia walikosoa kampeni za upotoshaji za Israel, wakiushutumu utawala huo vamizi ambao hueneza habari za uwongo na za kupotosha ili kuficha vitendo vyake vya kihalifu.

Mawaziri wa IOC walilaani jeshi katili la Israel kwa kuwalenga waandishi wa habari wa Palestina "kwa makusudi na kwa utaratibu", na kusisitiza kuwa hii ni sehemu ya kampeni ya "kunyamazisha sauti za wasema ukweli".

Taarifa hiyo pia ililaani vikosi vya Israel kwa kuvuruga mfumo wa mawasiliano ya simu katika Ukanda wa Gaza, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufungua "uchunguzi wa mara moja" kuhusu uhalifu huu na kuuwajibisha utawala wa Israel unaokalia ardhi za Palestina kwa mabavu.

Kwingineko katika taarifa yao, mawaziri hao wa habari wa nchi za Kiisalmu wamekariri kuwa "njia pekee ya amani na usalama katika eneo hili ni kupitia utambuzi wa haki zisizoweza kupokonywa za watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kitaifa na mamlaka huku Quds Mashariki ikiwa ni mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.

Akizugumza katika kikao hicho, Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran ametoa mwito wa kubuniwa mkakati maalumu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), utakaonakili jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Mohammad Mehdi Esmaili amesema ukusanyaji wa ushahidi madhubuti unaweza kusaidia kuwajibishwa na kubebeshwa dhima Israel kwa jinai na vitendo vyake visivyo vya kiutu dhidi ya Wapalestina.

Esmaili amebainisha kuwa, Iran inatoa mwito wa kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari miongoni mwa nchi wanachama wa OIC, kama sehemu ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza.Vita vya mauaji ya halaiki kati ya Marekani na Israel dhidi ya Gaza viko katika siku yake ya 143, huku mashambulizi ya anga na mizinga yakiendelea kwenye ukanda huo uliozingirwa. Takriban watu 30,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.