Saudia yaongoza katika kutupa chakula (israfu) duniani
Saudi Arabia inaongoza kwa israfu au kutupa chakula duniani huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula wakiwemo Wapalestina wa Gaza wanaokabiliwa na hujuma ya Israel.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Upotevu wa Chakula ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (UNEP), Saudi Arabia hutupa asilimia 50 kwa wastani ya chakula chote kinachotupwa ulimwenguni.
Waziri wa Mazingira, Maji na Kilimo wa Saudia, Abdul Rahman bin Abdul Mohsen Al Fadhli amethibitisha matokeo ya Umoja wa Mataifa huku akikiri nchi hiyo inapata hasara kubwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, israfu au upotevu wa chakula hugharimu ufalme wa Saudia dola bilioni 10.6 kila mwaka. Wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani serikali ya Saudia imezindua kampeni ya kuwahimiza wananchi kuacha kutupa chakula na wajifunze namna ya kutunza chakula kilichobakia.
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la Hefz Al-Nema katika eneo la Makka, Abdullah Osama Filali amesema taasisi hiyo imechukua hatua za kupunguza israfu ikiwa ni pamoja na kufanya makubaliano na hoteli, migahawa na kumbi za harusi ili kuchukua chakula cha ziada na kukigawa kwa wahitaji.
Barani Afrika, nchi tatu za juu zinazoongoza katika kutupa chakula ni Ushelisheli, Tunisia na Misri. Nchi zenye kiwango cha chini zaidi cha kutupa chakula ni Afrika Kusini, Zimbabwe na Botswana.
Umoja wa Mataifa umebaini kuwa wakati kiasi kikubwa cha chakula kinapotezwa kila siku, watu milioni 783 duniani wanakabiliwa na njaa kali.
Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP imesema, wakati theluthi moja ya watu duniani wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, milo bilioni moja, ambayo ni sawa na moja ya tano ya chakula chote hutupwa kila siku na kuishia jalalani.
Ripoti hiyo ya UNEP, ambayo imetolewa kwa anwani ya “Kielelezo cha Taka za Chakula 2024” inaangazia takwimu za hivi karibuni kuanzia mwaka 2022 ambazo zinaonyesha kuwa tani bilioni 1.05 za chakula zilipotea.