Congress ya Marekani inatumika kama ngao ya kumlinda Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111280-congress_ya_marekani_inatumika_kama_ngao_ya_kumlinda_netanyahu
Katika hali ambayo Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni lina wasiwasi mkubwa kuhusiana na uwezekano wa kutolewa waranti wa kukamatwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu na maafisa wengine wa utawala wa Kizayuni, tovuti ya habari ya Axios imeripoti kwamba wajumbe wa Congress wameionya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kuitaka isitoe vibali vya kutiwa nguvuni maafisa wa utawala wa Israel.
(last modified 2024-05-01T08:10:17+00:00 )
May 01, 2024 08:10 UTC
  • Congress ya Marekani inatumika kama ngao ya kumlinda Netanyahu

Katika hali ambayo Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni lina wasiwasi mkubwa kuhusiana na uwezekano wa kutolewa waranti wa kukamatwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu na maafisa wengine wa utawala wa Kizayuni, tovuti ya habari ya Axios imeripoti kwamba wajumbe wa Congress wameionya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kuitaka isitoe vibali vya kutiwa nguvuni maafisa wa utawala wa Israel.

Wajumbe wa Bunge la Marekani wameionya mahakama hiyo kwamba iwapo itatoa waranti wa kukamatwa maafisa wa Israel, itakabiliwa na jibu kali kutoka kwa Marekani. Awali, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel alimtaka Rais Joe Biden wa Marekani azuie waranti wa kukamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai.

Kwa mujibu wa gazeti la Haaretz, Karim Ahmad Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, anajiandaa katika kipindi cha siku chache zijazo kutoa waranti ya kukamatwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu, Yoav Galant Waziri wa Vita, na mkuu wa majeshi ya Israel.

Gazeti la Kiebrania la Yedioth Aharnot pia limeripoti, likimnukuu afisa mmoja wa Kizayuni, kwamba kuna uwezekano wa waranti ya kukamatwa maafisa wa utawala huo ikatolewa kwa siri na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya The Hague, na wahusika watafahamu suala hilo tu baada ya kusafiri nje ya ardhi zinazokaliwa kwa mbavu (Israel).

Kwa kuunda kundi maalum linalojumuisha mawakili na maafisa wakuu wa sheria wa utawala huo, kama vile Yariv Levin Waziri wa Sheria, Netanyahu anajaribu kuzuia kutolewa hukumu yoyote ya kimataifa dhidi ya maafisa wa kisiasa na makamanda wa kijeshi wa Israel na mahakama ya ICC.

Sehemu ya mauji ya halaiki yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina

Israel Kats Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni ametoa indhari kwa mabalozi na wanadiplomasia wa utawala huo kufanya maandalizi yanayohitajika ili kukabiliana na kuenea maandamano ya kimataifa dhidi ya sera za Netanyahu na jeshi la utawala huo endapo hukumu hiyo itatolewa. Wataalamu wa sheria za kimataifa wa utawala wa Kizayuni wametahadharisha juu ya kutolewa waranti za kukamatwa viongozi wa Israel na kusisitiza kuwa, suala hilo linaweza kusababisha vikwazo vingine vikiwemo vya kupigwa marufuku kuuziwa silaha Israel na vikwazo vingine vya kiuchumi. Kuhusiana na hilo, Wizara ya Sheria ya utawala wa Kizayuni inafanya juhudi kubwa ili kuzuia kutolewa waranti hizo.

Kwa kuzingatia hatua dhaifu za Jumuiya ya Kimataifa na taasisi za kisheria zenye uwezo katika kuzuia serikali ya mrengo wa kulia na yenye kupenda vita ya Israel na Netanyahu kufanya jinai za kivita huko Gaza, kutolewa waranti ya mahakama na kupewa kipaumbele utekelezaji wake ni hatua pekee  inayoweza kufanywa na  mahakama mbili za Kimataifa  ICC na ICJ ili kufuatilia kesi ya jinai na mauaji ya kimbari ya Israel.

Mahakama zote mbili zina hoja na ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa jinai za kivita na mauaji ya halaiki zimetendwa na utawala wa Tel Aviv na kwa msingi huo, juhudi za serikali na bunge la Marekani, za kuzuia kutolewa  hukumu katika mahakama hizo inazidi kutia nguvu nafasi ya nchi hiyo katika jinai za kivita huko Gaza.

Kama si himaya ya kijeshi na kisiasa ya Marekani kwa Israel, serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu haingeweza kudumisha kwa miezi 7 sasa vita vya Gaza. Katika siku za mwanzo wa vita vya Gaza, Marekani ilitoa msaada wa dola bilioni 14.3 kwa jeshi la utawala wa Kizayuni, na hivi karibuni iliongeza dola bilioni 30 nyingine kwa msaada huo, jambo ambalo lilikuwa halijawahi kushuhudiwa tena katika kipindi kifupi kama hiki. Hii ni pamoja na kuwa tokea mwaka 1948 Marekani imeipatia Israel dola zipatazo bilioni 263, ambapo dola bilioni 130 zilitolewa kama misaada ya kijeshi. Gazeti la Washington Post, likiwanukuu maafisa wa Pentagon na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, limeripoti kuwa kifurushi hicho kipya cha silaha kinajumuisha zaidi ya mabomu 1,800 ya Mark 84 na 500 ya Mark 82. Bomu la Mark 84 lenye uzito wa kilo 900 lilizungumziwa sana katika operesheni ya mauaji ya halaiki ya hivi karibuni yaliyofanywa na jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza. Marekani pia, kwa kutumia kura ya turufu, imezuia mara kadhaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea mashinikizo serikali ya Netanyahu ili isitishe vita na mauaji ya umati huko Gaza.

Vitisho vya Bunge la Congress kwa ajili ya kuzuia kutolewa waranti dhidi ya serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu vinatolewa katika hali ambayo sheria za ndani ya Marekani zinazuia kutolewa uungaji mkono wa kijeshi na kijasusi kwa hatua ambazo zinakiuka sheria za vita. Hii ni  kwa sababu ikiwa Israel itatumia usaidizi huo wa Marekani kutekeleza jinai za kivita, Marekani pia itachukuliwa kama mshiriki katika jinai hizo.

Ugaidi wa Israel dhidi ya watoto wa Palestina

Kwa kuzingatia suala hilo, Josh Paul, mmoja wa maafisa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambayo inasimamia uhamishaji wa silaha, alijiuzulu mwezi Oktoba kutokana na kuendelea kutumwa misaada ya kijeshi ya serikali ya Washington kwa Israel. Alisema katika mahojiano na gazeti la HuffPost kuwa "Imenithibitikia kwamba viongozi wengi  wa Marekani si tu kwamba wana habari kamilifu kuhusu jinsi Israel inavyotumia silaha za nchi hii katika vita vya Gaza, bali hata nyuma ya pazia wanayataja mashambulizi haya kuwa jinai za kivita."

Swali linalopaswa kuulizwa hapa ni kuwa je, ni kwa nini, licha ya vikwazo hivyo vya wazi vya kisheria, bunge la Congress na serikali ya Marekani bado zinaendelea kuiunga mkono Israel hata katika hali ya kutuhumiwa kuwa mshirika katika jinai za utawala huo? Jibu lake linapatikana katika maneno ya Jimmy Carter, rais wa zamani wa Marekani aliposema: "Mimi kama Mkristo pamoja na wengine wengi katika siasa za Marekani, tunaamini kanuni moja inayosema kwamba tunapasa kuunga mkono wakati wowote, chochote kile kinachofanywa na Israel na kuvifanya vyombo vya habari viwashawishi watu waunge mkono pia jambo hilo. Sisi tuna jukumu la kuunga mkono kivyovyote vile na wakati wowote sera za Israel."