Jinai baada ya jinai huko Gaza
Pamoja na kuwa Netanyahu anakabiliwa na hatari ya kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutokana na jinai kubwa za kivita anazofanya huko Gaza, lakini bado anaendelea kufanya jinai hizo bila kujali lolote kutokana na msaada na uungaji mkono mkubwa anaopata kutoka kwa Marekani.
Mashambulizi makali ya anga, nchi kavu na baharini ya utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo zima la Ukanda wa Gaza na hasa yale yaliyofanywa Jumatano alfajiri katika makazi ya wakimbizi wa Kipalestina katika ukanda huo yamepelekea makumi ya Wapalestina kuuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa.
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, ameelezea hali katika Ukanda wa Gaza kuwa "zaidi ya janga" na kusema katika Hospitali ya Kamal Adwan, mojawapo ya hospitali mbili zilizobaki kaskazini mwa Gaza, imekuwa vigumu zaidi kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa, ambapo makombora yamelenga na kuharibu kitengo cha huduma za dharura, na kuwalazimu madaktari na watoa-huduma kuwahamishia wagonjwa walio kwenye vitanda na machela kwenye barabara zilizojaa vifusi.
Mkurugenzi wa kanda wa Shirika la Afya Duniani pia amesema kuwa timu ya madaktari inayojumuisha watu 148 pamoja na wagonjwa 22 wamezingirwa katika Hospitali ya Al-Awda ambapo walenga shabaha wa Kizayuni wanafyatua risasi hospitalini hapo na pia makasha ya makombora yanayolipuliwa kuanguka kwenye majengo na uwanja wa hospitali hiyo.
Siku 229 zimepita tangu jeshi la Israel lianzishe vita vya mauaji ya umati huko Gaza ambapo jeshi hilo linalenga kiholela wanawake, watoto na wakimbizi bila kujali lolote. Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde za Wizara ya Afya ya Gaza, watu 35,647 wameuawa shahidi na wengine 79,852 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya wavamizi hao, ambapo miili ya zaidi ya watu 10,000 bado iko chini ya vifusi vya majengo na waokoaji wameshindwa kuifikia.
Katika duru ya mwisho ya mazungumzo, licha ya Hamas kukubaliana na mpango wa kusimamisha vita, lakini utawala wa Kizayuni ulikataa kuukubali mpango huo na badala yake ukaanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Rafah, ukidhani kwamba ungeweza kutumia operesheni hiyo kama chombo cha kuishinikiza Hamas ikubaliane na masharti yake ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka bila kufikiwa usitishaji vita wa kudumu na uondoaji wa vikosi vya uvamizi kutoka Gaza.
Utawala wa Kizayuni umekataa kuondoka katika vivuko vya mpaka wa Rafah ili kulifanya daraja la baharini lililojengwa Gaza na Wamarekani kwa malengo yasiyoeleweka vizuri, kuwa daraja pekee la kuunganisha eneo hili na ulimwengu wa nje. Majeshi ya Marekani yalikamilisha ujenzi wa "bandari inayoelea" kwenye pwani ya Gaza ili kuuwezesha utawala wa Israel uitumie kudhibiti usafiri wa watu wanaoenda na kutoka Gaza, suala ambalo linaondoa nafasi ya Misri kutumika kama lango pekee la kuingia na kutoka katika ukanda huo.
Mbali na vita kusababisha maafa na uharibifu mkubwa huko Gaza, pia vimezidi kudhoofisha uchumi wa Misri, ambapo serikali ya Cairo imelazimika kufanya mazungumzo ya kuiuzia Imarati mji wa Ras al-Hikmah na kufikia makubaliano ya kupewa mikopo mipya na IMF, Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya ili kudhibiti mashinikizo hayo ya kiuchumi.
Hii ina maana kwamba Marekani sio tu ni mshirika wa jinai za serikali ya mrengo wa kulia na inayopinga amani ya Netanyahu, bali kwa hakika imejitenga na madai ya kutoupendelea upande wowote katika uhusiano wake na Misri na Israel na kuupendelea zaidi utawala huo ghasibu, suala ambalo linaweza kuupa utawala huo unaopenda vita kupata kiburi na ujasiri wa kuanzisha mashambulizi ya kuteka ardhi za Misri na Jordan.