Imarati yaalani jinai za utawala wa Kizayuni katika mji wa Rafah
Wizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imelaani jinai za utawala wa kizayuni katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa kuna udharura utawala wa Kizayuni kufungamana na maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya ICJ.
Ofisi ya habari ya serikali ya Palestina Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita limeshambulia maeneo ya makazi ya wakimbizi wa Kipalestina zaidi ya 10 huko Rafah na kuwauwa shahidi Wapalestina zaidi ya 190.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati jana Jumatatu imetoa taarifa na kulaani mashambulizi endelevu ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yaliyopelekea kuuliwa shahidi na kujeruhiwa Wapalestina wengi huko Rafah.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati imesisitiza juu ya umuhimu wa kufikiwa mapatano ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza, kuwahami raia na kufungamana na utekelezaji wa maagizo kama yalivyoainishwa katika hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu kusitishwa haraka iwezekanavyo mashambulizi dhidi ya Rafah na kufunguliwa tena kivuko cha mji huo.