Israel yaendelea kumwaga damu za Wapalestina Jenin, Jabalia
Wakazi watano wa mji wa Jenin ni miongoni mwa makumi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kupigwa risasi na kushambuliwa kwa mabomu na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo mbali mbali ya Palestina jana Ijumaa.
Shirika la habari la WAFA limemnukuu Wissam Bakr, Mkrugenzi wa Hospitali ya Serikali ya Jenin akisema kuwa, Wapalestina hao waliuawa shahidi jana Ijumaa katika uvamizi wa wanajeshi makatili wa Israel dhidi ya kambi moja ya wakimbizi katika mji wa Jenin, kaskazini ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wizara ya Afya ya Palestina imewatambua Wapalestina hao waliouawa shahidi jana mjini Jenin kuwa ni Ahmed Bassem Al-Amouri (miaka 20), Qusay Amjad Hazouz, 23, Fouad Iyad Ashqar, 25, Yassin Al-Aridi (miaka 30), na Muhammad Mahmoud Jabareen, 54.
Shirika la habari la Palestina la WAFA limeripoti kuwa, wanajeshi makatili wa Kizayuni mbali na kutekeleza mauaji hayo ya kinyama, lakini pia wameharibu nyumba kadhaa na miundimbinu katika eneo hilo.
Wakati huo huo, televisheni ya al-Jazeera imeripoti kuwa, watoto watatu wa Kipalestina ni miongoni mwa watu watano waliouawa shahidi katika shambulio la anga la jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Jabalia, kusini mwa mji wa Khan Younis. Habari zaidi zinasema kuwa, wanandoa wawili pia waliuawa shahidi katika umwagaji damu huo wa Wazayuni huko Jabalia jana Ijumaa.
Aidha mapema jana, vikosi katili vya Wazayuni viliendeleza operesheni zao za nchi kavu katika kitongoji cha Shujayea, viungani mwa jiji la Gaza, ambapo vimetangaza kuua shahidi Wapalestina wasiopungua 100.
Tangu kuanza mauaji hayo ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, zaidi ya Wapalestina elfu 38,000 wameuawa shahidi na wengine karibu 90,000 kujeruhiwa.