Yemen yashambulia meli za US na Israel kwa makombora, droni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i113912-yemen_yashambulia_meli_za_us_na_israel_kwa_makombora_droni
Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya wanamaji na vya makombora vya nchi hiyo vimefanya operesheni nyingine dhidi ya meli tatu za kibiashara za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2024-07-10T23:02:10+00:00 )
Jul 10, 2024 23:02 UTC
  • Yemen yashambulia meli za US na Israel kwa makombora, droni

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya wanamaji na vya makombora vya nchi hiyo vimefanya operesheni nyingine dhidi ya meli tatu za kibiashara za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya nchi hiyo vimeshambulia kwa makombora meli hizo za mizigo zinazohusishwa na Marekani na Israel katika pwani ya taifa hilo la Kiarabu, ili kuwaunga mkono Wapalestina wakati huu ambapo Israel inaendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza kwa himaya ya Washington na waitifaki wake wa Magharibi.

Brigedia Jenerali Saree amesema meli ya kibiashara ya Marekani iliyolengwa kwenye operesheni hiyo ya makombora kadhaa ya balestiki katika Bahari Arabu, ina jina la Maersk Sentosa.

Aidha amesema meli nyingine zilizotwangwa kwa makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani za vikosi vya Yemen ni meli ya Marathopolis katika Bahari Arabu na meli ya MSC Patnaree katika Ghuba ya Aden. Meli hizo mbili zinahusishwa na utawala haramu wa Israel.

Brigedia Jenerali Saree

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Yemen amebainisha kuwa, shabaha zilizolengwa zilipigwa kwa usahihi akisisitiza kwamba mashambulizi hayo yamefanyika kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa huko Gaza; na kujibu hujuma za pamoja za Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen.

Amesema wanajeshi wa Yemen wataendelea na operesheni zao za kijeshi, na watazuia meli zinazomilikiwa na Israel au zile zinazoelekea katika  bandarini zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu hadi pale usitishaji vita wa kudumu utakapotekelezwa katika Ukanda wa Gaza.