Holocaust ya kukaririwa kila siku huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114146-holocaust_ya_kukaririwa_kila_siku_huko_gaza
Wazayuni wenye itikadi kali za kufurutu ada wanaotawala huko Tel Aviv, wakiongozwa na Benjamin Netanyahu, licha ya kushindwa kufikia malengo yao ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, wanaendelea kufanya mauaji mapya ya holocaust kila siku katika ukanda huo.
(last modified 2024-07-17T00:13:24+00:00 )
Jul 17, 2024 00:13 UTC
  • Holocaust ya kukaririwa kila siku huko Gaza

Wazayuni wenye itikadi kali za kufurutu ada wanaotawala huko Tel Aviv, wakiongozwa na Benjamin Netanyahu, licha ya kushindwa kufikia malengo yao ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, wanaendelea kufanya mauaji mapya ya holocaust kila siku katika ukanda huo.

Siku 285 zimepita tangu utawala wa kibaguzi uanzishe mauaji ya umati katika Ukanda wa Gaza, ambapo bado unaendelea kushambulia kinyama maeneo ya makazi ya raia yenye msongamano mkubwa wa watu katika ukanda huo. Siku ya Jumapili, Wapalestina 12 waliuawa shahidi na wengine 70 wakajeruhiwa katika shambulio la kijinai la utawala wa Kizayuni katika shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Unyama wa utawala wa Kizayuni katika mashambulizi ya mabomu katika eneo la al-Mawasi huko Khan Yunis, ambalo hapo awali lilitangazwa kuwa eneo salama kwa wakimbizi wa Kipalestina, umesababisha vifo na majeraha mabaya kwa watu zaidi ya 300. Jumuiya ya Kulinda Raia wa Ghaza ilitangaza Jumapili usiku kuwa, idadi ya mwisho ya mashahidi na waliojeruhiwa katika shambulio la utawala wa Kizayuni katika eneo la al-Mawasi siku ya Jumamosi ilikuwa watu 400.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huko Gaza alisema Jumapili usiku kwamba tangu kuanza vita vya Gaza, vituo 190 vya shirika hilo vimeharibiwa kabisa na utawala wa kigaidi wa Israel katika ukanda huo. Kabla ya hapo, Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema hakuna sehemu yoyote iliyo salama katika Ukanda wa Gaza na kutaka juhudi zaidi zifanyike kwa ajili ya kulinda usalama wa raia.

Mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina

 

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umetangaza kwamba familia nyingi katika eneo hilo zimelazimika kukimbia na kuhama mara kwa mara kutokana na hujuma ya kinyama inayofanywa na utawala wa Israel katika maeneo yao ya makazi. Shirika la Misaada na Uokoaji la Gaza pia limetangaza kuwa tangu kuanza uvamizi wa kijeshi wa Israeli katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba iliyopita hadi sasa, wafanyakazi wake wapatao 79 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya jeshi la utawala huo. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyombo vya Habari vya Michezo vya Palestina pia ametangaza kuwa tangu kuanza kwa vita vya Ghaza, wanamichezo 300 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni. Zaidi ya asilimia 90 ya vituo vya michezo vya mikoa ya kusini mwa Ghaza vimeharibiwa tangu kuanza uvamizi wa kijeshi wa utawala wa Israel katika ukanda huo.

Gazeti la The Guardian la nchini Uingereza limeripoti kuwa takriban tani milioni 40 za vifusi na taka zimerundikana katika Ukanda wa Gaza. Vyanzo vya kieneo katika Ukanda wa Gaza vinaelezea uharibifu mkubwa uliofanywa na Wazayuni huko Khan Younis kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Israeli ambayo yameharibu alama zote za uhai na maisha katika eneo hilo. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, tangu utawala huo aunzishe mauaji ya kimbari huko Gaza tarehe 7 Oktoba, zaidi ya Wapalestina elfu 38 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya elfu 88 wameuawa. Wale walionusurika kifo, hasa watoto na vijana wadogo, ambao ndio wakazi wengi wa Gaza, wanaishi katika hali mbaya na ya kusikitisha sana. Utapiamlo mkali umeenea miongoni mwa watoto huko Gaza, ambapo wengi wao wanakabiliwa na upungufu wa damu na shinikizo la chini la damu. Umoja wa Mataifa unasema idadi kubwa ya waliojeruhiwa na wanaokabiliwa na tatizo la utapiamlo imezidisha mashinikizo dhidi ya mfumo wa afya wa Gaza.

Ushahidi unaonyesha kuwa moja ya malengo ya utawala wa Israel ya kuzidisha jinai katika siku za hivi karibuni ni kukwamisha mazungumzo ya Doha yanayofautilia juhudi za kumaliza vita. Osama Hamdan, mmoja wa viongozi wa harakati ya Hamas amesema katika taarifa kwamba lengo la adui katika kushadidisha jinai dhidi ya watu wa Gaza ni kutoa mashinikizo katika mazungumzo ya Doha yanayofuatilia kuhitimisha vita huko Gaza. Mazungungumzo hayo yamevunjika kutokana na Waziri Mkuu wa Israel kuyavuruga kwa makududi jambo ambalo limewakasirisha sana washiriki wa mazungumzo hayo wakiwemo wa Israel, na hivyo kuweka wazi hitilafu kubwa zilizopo kati ya washiriki hao wa Israel na Netanyahu kuhusiana na suala zima la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Maandamano ya Waafrika Kusini ya kupinga jinai za Wazayuni huko Gaza

Kwa kutekelezwa mauaji ya kutisha ya hivi karibuni huko al-Mawassi, Wazayuni wamethibitisha kivitendo kwamba hawataki kabisa kusimamisha vita. Hii ni pamoja na kuwa hata baada ya kupita zaidi ya miezi 9 tangu utawala huo haramu ianzishe vita vya mauaji ya umati dhidi ya watu wa Gaza kwa kisingizio cha kuingamiza harakati ya muqawama ya Hamas na kuwarejesha nyumbani mateka wa Israel, lakini utawala huo haijafikia hata lengo moja kati ya malengo hayo. Kwa msingi huo, dhana hii imepata nguvu katika duru nyingi na hata miongoni mwa Wazayuni wenyewe kwamba Netanyahu amevuruga kwa makusudi mazungumzo ya Doha ili kuepusha kufuatiliwa kesi ya ufisadi inayomkabili katika mahakama za Israel na wakati huo huo kununua muda kabla Donald Trump hajaingia madarakani nchini Marekani ili apate kuunga mkono zaidi utawala wa Israel na kuushajiisha uendelee kufanya jinai za mauaji ya kimbari huko Gaza.