Shambulio la wanajeshi wa Israel kwenye Msikiti wa Al-Aqsa
Idara ya Wakfu wa Kiislamu ya Palestina katika mji wa Quds Tukufu unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel imetangaza kuwa wanajeshi wa utawala huo wamewazuia Waislamu kuingia katika eneo hilo takatifu kwa kuvamia Msikiti wa Al-Aqsa.
Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Baraza la Mawaziri la utawala wa Israel unaokalia kwa mabavu Palestina, na ambaye ana itikadi kali za Kizayuni ameingia katika Msikiti wa al-Aqsa akiwa ameandamana na wanajeshi wa utawala huo katili.

Kwa mujibu wa tangazo la Ofisi ya Wakfu wa Kiislamu ya Palestina katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utwala huo haramu, hii ni mara ya pili kwa waziri huyo wa Kizayuni mwenye misimamo mikali ya kupindukia mipaka kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa baada ya kuanza hujuma na mauaji ya kimbari ya utawala huo ghasibu katika Ukanda wa Gaza.
Waziri huyo mwenye itikadi kali wa utawala wa Kizayuni ameuvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqsa katika hali ambayo utawala huo unaendesha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana, ambapo zaidi ya Wapalestina 38,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 89,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama.