UNICEF: Asilimia 90 ya wakaazi wa Gaza wamekimbia makazi yao
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, asilimia 90 ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza wameyakimbia makazi yao baada ya hujuma na uvamizi wa jeshi la Israel dhidi ya eneo hilo.
Ripoti ya Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imesisitiza kuwa, wakimbizi wengi wa Kipalestina ambao wameyahama makazi yao tangu kuanza kwa vita vya Gaza (Oktoba 2023) ni watoto na wanawake.
Philippe Lazzarini, Mkurugenzi wa Shirika la Ajira na Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), alitangaza pia hivi karibuni kwamba utawala wa Israel kwa akali umezishambulia kwa mabomu shule 8 za Ukanda wa Gaza katika muda wa chini ya wiki mbili, 6 kati yake ni za UNRWA.
Wakatii huo huo, idadi ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa tangu kuanza hujuma kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza (Oktoba 7) imekaribia watu 39,000.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, zaidi ya wafanyakazi 300 wa sekta ya afya, vikosi 35 vya ulinzi wa raia na wafanyakazi 135 wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wameuawa shahidi katika hujuma inayoendelea ya utawala ghasibu wa Israel.
Uungaji mkono wa wazi wa Marekani na nchi za Magharibi umepelekea kushuhudiwa faili jeusi la viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanaoua watu wasio na ulinzi wala hatia. Bila shaka wale wote wanaohami na kuunga mkono jinai za Israel wanahusika pia katika jinai na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.